Home Uncategorized AMANA BENKI NA TY SERVICES LIMITED ZA SAINI MKATABA KUWEZESHA MADEREVA WA...

AMANA BENKI NA TY SERVICES LIMITED ZA SAINI MKATABA KUWEZESHA MADEREVA WA TAXIFY NCHINI KUMILIKI VYOMBO VYA MOTO

963
0

Na Abraham Ntambara, Dar es Salaam

AMANA Benki na TY Services Limited ambayo ni kampuni inayoendesha mtandao wa Taxify nchini zimesaini mkataba wa kuwawezesha madereva wa Taxify kumiliki vyombo vya moto (Motor Vehicle Financing Scheme).

Meneja Kitengo cha Biashara Amana Benki Dassu Mussa (kushoto) na Meneja wa Taxify nchini Remmy Esake (kulia) wakiwa wameshikana mikono baada ya kusaini mkataba huo jijini Dar es Salaam.

Akizungumza leo jijini Dar es Salaam wakati wakutiliana saini mkataba huo, Meneja Kitengo cha Biashara wa Amana Benki Dassu Mussa, alisema lengo ni kuboresha usafiri na kuwaongezea madereva kipato kwa kuwawezesha kumiliki vyombo vya moto.

“Kwa upande wa Amana Benki kama benki inayoendeshwa kwa kuzingatia misingi ya kiislam hatua hii ni sehemu ya mikakati ya kuifanya benki hii kuwa kiongozi katika kutoa huduma za kibunifu zinazolenga kuinua jamii kiuchumi,” alisema Mussa.

Alibainisha kwamba uwezeshaji huo utafanyika katika vikundi, hivyo madereva watahitajika kuunda kikundi cha madereva 10 ambao watadhaminiana wenyewe.

“Dereva atatakiwa kuweka amana isiyopungua asilimia 10 ya thamani ya chombo cha moto anachohitaji kuwezeshwa, amana hii itatumika kama dhamana mpaka dereva atakapomaliza kufanya marejesho,” alisema.

Alieleza kuwa dereva atatakiwa kuweka akiba ya sh. 15,000 kila wiki ambayo itakuwa kama dhamana mpaka dereva atakapomaliza kufanya marejesho.

Mussa aliongeza, dereva atafanya marejesho kulingana na makubaliano na benki katika kipindi kisichozidi miaka miwili na kwamba benki itazingatia vigezo mbalimbali katika kutoa uwezeshaji huo ikiwemo dereva kuwa na uzoefu wa kutosha na rekodi nzuri.

Aidha alisema ni matarajio yao madereva wa Taxify watachangamkia fursa hii ili kuweza kumiliki vyombo vyao vya usafiri na kujiongezea kipato.

Kwa upande wake Meneja wa Taxify nchini Remmy Esake alisema mkataba huo utakuwa chachu ya kuhakikisha wanatoa huduma bora za usafiri na kwa gharama nafuu.

Aliwataka madereva kuchangamkia fursha hiyo ili waweze kumiliki vyombo vya moto vitakavyowasiadia kuwaingizia kipato na kuimarika kiuchumi.

Pichani ni matukio katika picha wakati wa utilianaji saini mkataba huo baina ya Amana Benki na TY Services Limited.