Home Michezo CAF yamzuia Hassan Kessy Dar

CAF yamzuia Hassan Kessy Dar

44
0

CAF yamzuia Hassan Kessy Dar

Achana na matokeo ya juzi ya Ligi Kuu Bara kati yao na Kagera Sugar, Yanga imesema bado ina matumaini ya kupindua meza mjini Gaborone, Botswana watakapoenda kuivaa Township Rollers, lakini CAF imewatibulia.

Shirikisho hilo la Soka Afrika (CAF) limemzuia beki aliye kwenye ubora wake kwa sasa, Hassan Kessy kwenda Gaborone kuivaa Township, kutokana na kuwa na kadi mbili za njano.
Kessy anayemfuata kwa karibu nahodha msaidizi wa Yanga, Kelvin Yondani kwa ubora ndani ya kikosi hicho kiasi cha kurudishwa kwenye kikosi cha Taifa Stars, hataruhusiwa kucheza mchezo huo na CAF imewajulisha Yanga mapema.

Meneja wa Yanga, Hafidh Saleh alisema imejulishwa kwamba Kessy hataruhusiwa kucheza mechi hiyo kutokana na kuzuiwa na kanuni.

Alisema Kessy alipata kadi ya kwanza katika mchezo wa marudiano nchini Shelisheli dhidi ya St Luois kisha nyingine dhidi ta Township Rollers ya Botswana jumanne wiki hii.

“Tumeshaambiwa hatuwezi kumtumia Kessy katika mchezo wa marudiano, amefikisha kadi mbili za njano. Wachezaji wengine wako vizuri hakuna mwenye tatizo kama hilo, lakini tuna watu wa kuziba nafasi yake,” alisema Saleh aliyedumu na Yanga kwa muda mrefu katika nafasi hiyo.
Tayari kocha, George Lwandamina ameanza kumuandaa beki mkongwe Juma Abdul kuziba nafasi ya Kessy.

Katika mechi yao ya kwanza iliyopigwa wikiendi iliyopita, Yanga ililala mabao 2-1 na kuwa na mlima wa kupanda wakati watakaporudiana wiki ijayo, ikihitaji kushinda ili kutinga makundi ya Ligi ya Mabingwa.

Source : Mwanaspoti