Home News CDF NA ISDI WATUMIA BONAZA KUHAMASISHA NAFASI YA WANAUME NA VIJANA KATIKA...

CDF NA ISDI WATUMIA BONAZA KUHAMASISHA NAFASI YA WANAUME NA VIJANA KATIKA KUTETEA HAKI, ULINZI NA USTAWI WA WATOTO

1622
0

 

Timu ya Bodaboda ya Kitunda
 

 

Afisa Ushirikishaji Wanaume na Vijana wa CDF Kiswigo Mwango’onda akizungumza kwenye bonanza lililofanyika katika kiwanja cha shule ya msingi Kitunda jijini Dar es Salaam.


 Afisa Ustawi wa Jamii kutoka Manispaa ya Ilala Joyce Maketa, akikagua tibu zilizoshiriki katika bonanza hilo  katika kiwanja cha shule ya msingi Kitunda jijini Dar es Salaam.


Mwakilishi kutoka ISDI Dk. Jonas Tiboroha akizungumza kwenye bonanza lililofanyika katika kiwanja cha shule ya msingi Kitunda jijini Dar es Salaam.

Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam

SHIRIKA la Jukwaa la Utu wa Mtoto (CDF) kwa kushirikiana na Taasisi ya Intercultural Sports Development Initiative (ISDI) wamefanya bonanza lenye lengo la kuhamasisha wanaume na vijana katika kutetea haki, ulinzi na ustawi wa watoto.

Kwa ufadhili wa Shirika la Maendeleo la Uswidi (Sida), bonanza hilo la mchezo wa mpira wa miguu lilifanyika jana kwenye kiwanja cha shule ya Msingi Kitunda, wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam, likishirikisha timu za waendesha bodaboda Kitunda (SanLG Bodaboda) na Kitunda United zote kutoka Kata ya Kitunda.

Akizungumza wakati wa bonanza hilo Afisa Ushirikishaji wa Wanaume na Wavulana kutoka CDF Kiswigo Mwang’onde, alisema wamefanya hivyo ili kushirikisha wanaume na vijana kwa kutambua nafasi yao katika kukomesha vitendo vya ukatili.

“Lengo la bonanza hili ni kujadili nafasi ya wanaume na wavulana katika kukomesha ukatili dhidi ya wanawake na watoto ili kupata jamii inayojali usawa wa kijinsia,” alisema Mwang’onde.

Aliongeza kwamba bonanza hilo pia lilikua na umuhimu katika kuwasilisha jumbe mbalimbali zenye kuhamasisha wanaume kushiriki malezi ya watoto na kukomesha aina zote za ukatili wa kijinsia.

Kwa Upande wake fisa Ustawi wa Jamii kutoka Manispaa ya Ilala Joyce Maketa, aliwapongeza wadau hao kwa kufanya bonanza hilo na kuwakusanya wanaume na wavulana pamoja na kuwapa ujumbe mzito na muhimu kwa ajili ya kumlinda mtoto wa kike.

Alisema kuwa kata ya Kitunda ni miongoni mwa maeneo yanayokabiliwa na changamoto zinazochangia kwa mtoto wa kike kukosa haki zake ambapo alitaja baadhi ya changamoto hizo kuwa ni suala la ukeketaji, ulawiti na ubakaji.

“Lakini hili shirika la CDF kwa kipindi kirefu limekuwepo hapa na limetusaidia kuhakikisha jamii inafikiwa na ujumbe huu, kwa wao kufanya bonanza hili mimi kwangu ni kitu kikubwa sana kwa sababu naona linaongeza wigo wa jamii kupata taarifa zinazohusu mtoto wa kike,” alisema Maketa.

Naye mwakilishi wa ISDI Dk. Jonas Tiboroha alisema wameamua kushirikiana na CDF katika bonanza hilo kutokana na taasisi yao kuwa na malengo makuu matatu ambayo yote yamejikita katika kusaidia jamii hususani vijana wakike na kiume kufikia ndoto zao.

Hata hivyo Nahodha wa timu ya Kitunda United Omary Suleiman, alisema lengo la bonanza hilo ni zuri na kuiomba serikali na wadau wengine kusaidia katika kutoa elimu juu ya masuala hayo kwani itasaidia kutokomeza janga hilo.

Aidha alitoa wito kwa CDF kuhakikisha linafanya mambonanza mengine mikoani hususani vijijini ambapo ndipo masuala ya ukatili yalipokithiri kwani jamii vijijini itakapofikiwa na kupatiwa elimu itasaidia kukomesha tatizo hilo.

Bonanza lilibebwa na Ujumbe juu ya nafasi ya wanaume na vijana katika kukomesha ukatili wa kijinsia na liliambatana na mafunzo juu ya madhara ya ukatili dhidi ya watoto pamoja na burudani ya mechi ya mpira wa miguu na muziki wa singeli kutoka kwa msanii Philemon Augustino (Yuda Msaliti) .

Katika bonanza hilo matokeo ni kwamba timu ya Kitunda United iliibuka mshindi kwa goli 1-0 dhidi ya waendesha bodaboda wa Kitunda (SanLG Bodaboda).

 

 Picha ya pamoja  timu pamoja na viongozi