Home News GESI BADO INA NAFASI KUBWA KATIKA KUCHANGIA PATO LA TAIFA – NAIBU...

GESI BADO INA NAFASI KUBWA KATIKA KUCHANGIA PATO LA TAIFA – NAIBU WAZIRI

1608
0
         Na Veronica Simba – Dodoma
Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu, amesema kuwa gesi asilia inayopatikana nchini, ingali na nafasi kubwa ya kuchangia katika Pato la Taifa, tofauti na hofu ya baadhi ya watu kuwa Serikali haiipi tena kipaumbele sekta hiyo.
 
Alitoa kauli hiyo jana, Septemba 9, 2018 jijini Dodoma, wakati akijibu hoja za wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, walizoziwasilisha katika semina maalum iliyoandaliwa na Wizara kuhusu masuala ya umeme, mafuta na gesi asilia.
 
Awali, wakitoa maoni na hoja mbalimbali wakati wa semina hiyo, baadhi ya wajumbe wa Kamati hiyo, walionyesha wasiwasi wao kuwa Serikali hailipi tena kipaumbele suala la gesi asilia kama ilivyokuwa miaka kadhaa iliyopita.
 
“Serikali haijabadili msimamo na mtazamo wake kuhusu gesi asilia hata kidogo. Ndiyo maana Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) limepewa dhamana ya kufanya kazi kibiashara ambapo pamoja na mambo mengine, linashughulika na biashara ya gesi ili kukuza mchango wake katika Pato la Taifa,” alifafanua Naibu Waziri.
 
Akifafanua zaidi, alisema kwamba, miradi mbalimbali ya gesi asilia inaendelea hivi sasa ambayo ni pamoja na uunganishaji wa gesi katika kiwanda cha saruji cha Dangote, katika viwanda vikubwa vilivyopo Mkuranga pamoja na kuunganisha majumbani.
 
Aidha, alisema, Mpango Mkakati wa matumizi ya gesi asilia umeainisha ni kiwango gani cha gesi kitatumika katika viwanda vya mbolea, viwanda vya kawaida na katika matumizi ya majumbani.
Hata hivyo, Naibu Waziri alibainisha kuwa, umuhimu wa gesi asilia kwa Taifa, haundoi umuhimu wa vyanzo vingine mbalimbali vya nishati ambavyo Tanzania imejaaliwa kuwa navyo vikiwemo vya maji, jotoardhi, upepo, tungamotaka na kadha wa kadha.
 
“Lengo la Serikali ni kuhakikisha tunavitumia ipasavyo vyanzo vyote hivyo tulivyonavyo, kila kimoja kwa nafasi yake ili tuweze kuzalisha nishati ya kutosha itakayoleta tija kwa wananchi na Taifa letu kwa ujumla.”
 
Akizungumzia Miradi ya uzalishaji umeme ambayo kwa sasa Serikali imeelekeza nguvu zaidi, alisema ni pamoja na ule wa kuzalisha umeme kwa kutumia maporomoko ya maji ya Mto Rufiji, ambao alisema, ukikamilika utaleta tija kubwa kwa Taifa.
 
Kuhusu hofu inayozungumzwa na baadhi ya watu kuwa, utekelezaji wa Mradi huo utaleta changamoto nyingi; Naibu Waziri aliwahakikishia wawakilishi hao wa wananchi kuwa, Taarifa ya wataalam kuhusu Athari za Kimazingira (EIA), imebainisha kuwa faida za Mradi endapo utatekelezwa ni kubwa sana ukilinganisha na changamoto, ambazo ni chache.
 
Semina hiyo kwa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini ilikuwa ya siku mbili na ilihitimishwa jana.
PIC%2B1
 Naibu Waziri wa Nishati Subira Mgalu, akizungumza wakati wa Semina ya Wabunge wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini (hawapo pichani), kuhusu masuala ya umeme, mafuta pamoja na gesi. Semina hiyo ya siku mbili iliandaliwa na Wizara ya Nishati ambapo ilihitimishwa jana, Septemba 9, 2018 jijini Dodoma
PIC%2B2
 Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Dkt. Hamisi Mwinyimvua, akizungumza wakati wa Semina ya Wabunge wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini (hawapo pichani), kuhusu masuala ya umeme, mafuta pamoja na gesi. Semina hiyo ya siku mbili iliandaliwa na Wizara ambapo ilihitimishwa jana, Septemba 9, 2018 jijini Dodoma.
PIC%2B3
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Dustan Kitandula, akizungumza wakati wa Semina iliyoandaliwa na Wizara ya Nishati kwa Wajumbe wa Kamati hiyo (hawapo pichani), kuhusu masuala ya umeme, mafuta pamoja na gesi. Semina hiyo ya siku mbili ilihitimishwa jana, Septemba 9, 2018 jijini Dodoma.
PIC%2B4
Meza Kuu – Kutoka kulia ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati Dkt. Hamisi Mwinyimvua, Naibu Waziri wa Nishati Subira Mgalu, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini Dustan Kitandula na Kaimu Katibu wa Kamati Agnes Nkwera, wakiwa katika Semina iliyoandaliwa na Wizara ya Nishati kwa Wajumbe wa Kamati hiyo (hawapo pichani), kuhusu masuala ya umeme, mafuta pamoja na gesi. Semina hiyo ya siku mbili ilihitimishwa jana, Septemba 9, 2018 jijini Dodoma.
PIC%2B5
PIC%2B6
Baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, wakichangia hoja na kutoa maoni wakati wa Semina iliyoandaliwa na Wizara ya Nishati kwa Wajumbe wa Kamati hiyo kuhusu masuala ya umeme, mafuta pamoja na gesi. Semina hiyo ya siku mbili ilihitimishwa jana, Septemba 9, 2018 jijini Dodoma.
PIC%2B7
PIC%2B8
PIC%2B9
PIC%2B10
PIC%2B11
PIC%2B12
PIC%2B13

Sehemu ya washiriki wa Semina iliyoandaliwa na Wizara ya Nishati kuhusu masuala ya umeme, mafuta pamoja na gesi kwa Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, wakiwemo Wabunge, Viongozi na Maafisa waandamizi kutoka Serikalini, wakiwa katika Semina hiyo ya siku mbili ambayo ilihitimishwa jana, Septemba 9, 2018 jijini Dodoma.