HIZI NDIZO Dawa rasmi za kuongeza nguvu za kiume - The Choice

HIZI NDIZO Dawa rasmi za kuongeza nguvu za kiume

0
Upset couple finding out results of a pregnancy test

Upset couple finding out results of a pregnancy test

Hatimaye Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA), imeibuka na kueleza wazi kuwa dawa pekee zinazofaa ni zile zilizothibitishwa kitaalamu kuwa zinafaa kwa matibabu hayo na siyo vinginevyo.

Kuwapo kwa utitiri wa matangazo holela ya dawa za nguvu za kiume, hasa katika maeneo ya mijini ikiwamo jijini Dar es Salaam na ndio kulisababisha kuweo kwa nia ya kutambua dawa rasmi zilizothibitishwa na TFDA na wala hazizidi tano.

Nyingine nyingi hazijathibitishwa na hivyo kuwa na uwezekano wa kutotimiza matarajio ya watumiaji au kuwahatarisha na madhara mbalimbali, yakiwamo ya kupasuka kwa mishipa ya damu iliyopo kwenye moyo.

Afisa Uhusiano wa TFDA, Gaudensia Simwanza, alisema kwamba, ni kweli kuna dawa nyingi zinazotangazwa na watu mbalimbali kuwa zinatibu tatizo la nguvu za kiume, lakini zilizo rasmi ni pamoja na Viagra, Erecto, Cialis na Suagra.

Simwanza alisema dawa hizo ndizo wanazozitambua kuwa zinaweza kutumiwa na watu waliopungukiwa au kuishiwa kabisa nguvu za kiume, kwa sababu zimepitishwa baada ya kukidhi vigezo vya kitaalamu. Hata hivyo, Simwanza alisema dawa hizo siyo za kutumiwa kiholela bali wenye shida nazo ni lazima wafuate maelekezo ya madaktari ili kujiepusha na madhara yake pindi zikitumika kiholela.

“Kuna dawa nyingi ambazo sisi tunazitambua na tumezipitisha zitumike, lakini mtu asizitumie hadi pale atakapopewa ushauri wa daktari. Hizi zina nguvu sana na zinaweza kufanya mishipa ya moyo kupasuka ama kuathiri mfumo wa damu kwa watu wanaozitumia bila kufuata maelekezo ya madaktari,” alisema Simwanza.

Alipoulizwa kuhusu dawa za asili za kuongeza nguvu za kiume, zikiwamo maarufu za kizizi cha mkuyati na zile zinazofahamika kama vumbi la Kongo, zikihusisha orodha ya dawa mbalimbali za aina hiyo kutoka Kongo zikiwamo za kasongo na mundende, Simwanza alisema TFDA hawawezi kuzizungumzia hizo na badala yake waulizwe wataalamu wa kitengo cha Tiba Asili na Tiba Mbadala cha Wizara ya Afya.

Dawa nyingine maarufu za kiasili ambazo huuzwa katika maeneo mbalimbali jijini Dar es Salaam, hutambulishwa kwa majina ya mkongoraa, sheki na oljanilolo inayopatikana zaidi kwa morani wa Kimasai.

Alipoulizwa kuhusu dawa hizo za asili kwa ajili ya kushughulikia tatizo la nguvu za kiume, Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Tiba Asili na Tiba Mbadala katika Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Paul Mhame, alisema hivi sasa Wizara ya Afya iko katika utaratibu wa kusajili dawa za asili zikiwamo hizo (kizizi cha Mkuyati na jamii ya vumbi la Kongo) ikiwa zitathibitika kuwa zinafaa na hazina madhara kwa watumiaji.

Akieleza zaidi, Dk. Mhame alisema kuwa hadi sasa hakuna dawa ya asili yoyote ambayo imesajiliwa na Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala na kwamba, kwa sababu hiyo, hakuna dawa ya kiasili ambayo Wizara inaweza kuizungumzia kwa uwazi kuwa imethibitishwa kuwa inaongeza nguvu za kiume pasi na kuwa na madhara yoyote kwa watumiaji.

Dk. Mhame aliongeza kuwa kwa sababu hiyo ya kutokuwapo kwa usajili rasmi kwa dawa za asili hadi kufikia sasa, ni vyema watumiaji wakawa waangalifu kutumia dawa za namna ya kizizi cha Mkuyati na vumbi la Kongo zinazouzwa kiholela mitaani kwa sababu zinaweza kuwasababishia madhara makubwa kiafya kwa vile ni dawa ambazo hazina vipimo sahihi vya matumizi yake.

Hata hivyo, Dk.Mhame alikiri kuwa Tanzania ina miti mingi ya asili ambayo inaweza kutumika kutibu masuala ya tendo la ndoa baina ya wapendanao, lakini ni muhimu kutambua kuwa tiba inapotangazwa kwa sura ya kibiashara inatia shaka na hivyo watumiaji wanapaswa kuwa macho.

“Kwa mfano, kuna watu wanauziwa kile wanachoelezwa kuwa ni supu ya pweza mitaani kuboresha afya zao hasa kuhusu nguvu za kiume… lakini ni muhimu kuwa waangalifu ili kujiridhisha kuwa kweli kinachouzwa na watu kunywa ni supu ya pweza au ni maji tu ya kawaida,” alitahadharisha Dk. Mhame.

Aliongeza kuwa zipo dawa kadhaa za tiba asili ambazo baraza wanazitambua kuwa husaidia kutatua tatizo la nguvu za kiume, lakini nyingi hazifanyi kazi za papo kwa papo kama watu wanavyoaminishwa, bali nyingi humlazimu mhusika atumie dawa hizo kwa siku akdhaa ili mwili urudi katika hali yake ya awali na kupata jawabu ya kile kinachotarajiwa.

Alisema kuwa, ipo mimea imethibitika pia kutatua tatizo la nguvu za kiume kama mahama au mapama, ubuyu na majani ya mlonge, lakini zote hizo humsaidia mtu aliyepungukiwa na nguvu za kiume kurudisha mwili wake katika hali ya kawaida baada ya dawa hizo kutumiwa kwa siku kadhaa na siyo papo kwa papo, kama inavyoelezwa kuhusu kizizi cha mkuyati na vumbi la Kongo.

Aliongeza kwa kusema, ili dawa ya tiba asili ifanye kazi papo kwa papo, ni lazima ikamuliwe na kuondolewa viambata vingine ndipo itafanya kazi papo kwa papo kama ilivyo kwa dawa aina ya Viagra, lakini muhimu ni kufuata maelekezo ya daktari.

Facebook Comments
Share.

About Author