Home News KAMISHNA TRA AWAASA WAKULIMA, WAFANYABIASHARA KUTUMIA MASHINE ZA EFD

KAMISHNA TRA AWAASA WAKULIMA, WAFANYABIASHARA KUTUMIA MASHINE ZA EFD

85
0

Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania, Bw. Charles Kichere akijadili jambo na Bi.Magdalena Faustine Shirima, Afisa kutoka Kliniki ya Biashara Tanzania(TanTrade) alipotembelea kliniki hiyo katika Viwanja vya Nane Nane-Nyakabindi, Mkoani Simiyu.

Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania, Bw. Charles Kichere akimkabidhi mfanyabiashara wa Simiyu Bw. Saidi Mussa Namba ya Utambulisho wa Mlipakodi (TIN) na mashine ya kutolea risiti za kielektroniki.

Na Mariam Mwayela
Nyakabindi, Simiyu
Kamishna wa Mamlaka ya Mapato Tanzania, Bw. Charles Kichere amewaasa wakulima na wafanyabiashara wote kulipa kodi stahiki na kutumia mashine za risiti za Kielektroniki pindi wanapouza ama kununua bidhaa kutoka kwa wafanyabiashara wenzao.
Akizungumza na baadhi ya wananchi na waandishi wa habari waliotembelea banda la TRA katika Maonesho ya Nane Nane-Nyakabindi Mkoani Simiyu, Kamishna Mkuu amesema kuwa maendeleo ya nchi na shughuli za serikali kwa asilimia kubwa zinategemea kodi, hivyo kila wananchi wanatakia kuchangia kwa kulipa kodi.
“Kodi tunayolipa inafanya kazi kubwa sana na ndo mana tunaona wanafunzi wengi wanadahiliwa katika vyuo vikuu, reli ya kisasa ya SGR inatengenezwa, madawa yanapatikana kwa wingi katika hospitali zetu pamoja na huduma mbalimbali za kiuchumi na kijamii kupatikana kwa urahisi”, alisisitiza Kichere
Bw. Kichere aliongeza kuwa, Serikali kwa kutambua umuhimu wa kodi imeendelea kufanya juhudi mbalimbali za kuhakikisha kila mfanyabiashara anayestahili kulipa kodi anafanya hivyo kwa kupunguza Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwenye mashine za EFD.
“Mashine za EFD zilikuwa zinauzwa kwa Shilingi 690,000/= lakini sasa zinapatikana kwa shilingi 590,000/= ili kila mfanyabiashara atumie mashine hizi”, aliongeza Kichere.
Bw. Kichere aliwahakikishia wafanyabiashara kuwa serikali imeweka Mpango Mkakati wa kuhakikisha mashine za EFD zinatengenezwa hapa hapa nchini na tayari baadhi ya wawekezaji wameonyesha nia ya kutaka kuwekeza kutokana na uhitaji wa mashine hizo kuwa mkubwa.
“Mashine zikitengenezwa hapa nchini zitakuwa na bei ya chini zaidi kwa kila mfanyabiashara kuweza kununua, uwepo wa viwanda vya kutengeneza mashine za EFD kutaunga mkono juhudi za Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa John Pombe Magufuli kuelekea Tanzania ya viwanda”, alisema Kichere.
Kamishna Mkuu alitoa wito kwa wafanyabiashara na wananchi kwa ujumla kulipa kodi stahiki kwa mujibu wa sheria, na kuwaomba wananchi kutokuwafumbia macho wafanyabiashara wanao kwepa kulipa kodi kwa namna moja ama nyingine ikiwemo kutokutoa risiti za mashine za kielektroniki pindi wanapouza bidhaa au huduma na wananchi kuhakikisha wanadai risiti za mashine za Kielektroniki pindi wanaponunua bidhaa au huduma.
Kwa upande wake Bw. Saidi Mussa, mfanyabiashara wa Mkoa wa Simiyu aliyefika banda la TRA kuweza kupatiwa Namba ya Utambulisho wa Mlipakodi na kununua mashine ya risiti ya kielektroniki alisema amehamasika kufanya hivyo kutokana na juhudi za serikali kuhamasha na kuelimisha kuhusu masuala ya kodi.
“Nimeelewa kuhusu umuhimu wa kodi kutokana na elimu mbalimbali inayotolewa hivyo nimeamua nimuunge mkono Mheshimiwa Rais, John Pombe Magufuli kwa kulipa kodi kwa hiyari na kutumia mashine za EFD’’, alisema Saidi.
Mamlaka ya Mpato Tanzania inashiriki Maonesho ya 25 ya Sikukuu ya Wakulima ya Nane Nane Kitaifa Mkoani Simiyu pamoja na mikoa ya Arusha, Lindi, Morogoro pamoja na Mbeya ambapo huduma mbalimbali zinatolewa ikiwepo huduma ya Namba ya Utambulisho wa Mlipakodi, Elimu ya Kodi hususani katika faida na umuhimu wa kulipa kodi, kodi ya majengo  pamoja na matumizi ya mashine za kielektroniki.