Home News KASI ZAIDI YATAKIWA KUSIMAMIA SEKTA YA UVUVI

KASI ZAIDI YATAKIWA KUSIMAMIA SEKTA YA UVUVI

1836
0
Na. Edward Kondela
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega amekutana na Waziri wa Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mhe. Rashid Ali Juma, Mjini Unguja na kumweleza kuwa serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inahakikisha miradi inayohusu wavuvi inawanufaisha moja kwa moja.
Katika mazungumzo hayo ambayo pia yamehudhuriwa na Naibu Waziri wa Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mhe. Makame Ali Ussi, Naibu Katibu Mkuu wa wizara hiyo Bw. Islam Seif Salum pamoja na watendaji wengine wizara, Mhe. Ulega amesema lengo kuu la ziara yake ya siku moja kisiwani Zanzibar ni kutazama shughuli za Mamlaka ya Usimamizi wa Bahari Kuu Zanzibar kupitia mradi wa Usimamizi wa Uvuvi Kusini Magharibi mwa Bahari ya Hindi (SWIOFISH).
“Tunahitaji tuone rasilimali za bahari zinatunufaisha, mchango wake bado ni mdogo sana mradi wa SWIOFISH una pesa nyingi lakini bado hatujaona mafanikio ya moja kwa moja kuwasaidia wananchi tulikubaliana kuna mambo ya kurekebisha.” Alisema Mhe. Ulega
Kwa upande wake Waziri wa Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mhe. Rashid Ali Juma amesema uchafuzi wa bahari, uwepo wa maharamia na uvuvi haramu ni mambo ambayo Serikali ya Mapinduzi Zanzibar inaendelea kukabiliana nayo ili kuhifadhi bahari na kufanya sekta ya uvuvi kuwa yenye tija kwa wananchi.
Mhe. Juma pia amesema Serikali ya Mapinduzi Zanzibar itaendelea kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika masuala yanayohusu uvuvi ili kubadilishana uzoefu hasa baada ya hivi karibuni kuhudhuria mkutano wa “Blue Economy” nchini Kenya ambapo nchi washiriki wa mkutano huo walikubaliana kusimamia mambo mbalimbali ili kulinda rasilimali za Bahari ya Hindi.
Mara baada ya mazungumzo hayo, Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega alipata fursa ya kukutana na watendaji wa wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi wa Serikali ya Mapinduzi pamoja na watendaji wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bahari Kuu Zanzibar ambapo amewataka kujenga mazingira ambayo yatawanufaisha wavuvi hususan kwa kubuni teknolojia za kisasa kwa ajili ya shughuli za uvuvi.
“Unajua viongozi wetu wanataka kuona tunakuja na vitu gani vipya, mapinduzi gani mapya, tusikae na sisi tukaendelea kufanya vile vile kwa maana shughuli za uvuvi za kurithishana, jukumu letu viongozi ni kuwasaidia wavuvi hawa kupata teknolojia ili kuwarahisishia shughuli zao badala ya sasa wakiendelea kuvua kwa kubahatisha.” Alisema Mhe. Ulega
Aidha Mhe. Ulega ametoa wito kwa watendaji hao kutumia vizuri fedha zilizotolewa na Benki ya Dunia Shilingi Bilioni Tano kwa ajili ya mradi wa SWIOFISH ili kuleta mapinduzi ya kweli katika sekta ya uvuvi na kuhakikisha wanafanyakazi kwa kasi kulingana na matarajio ya serikali zote mbili kwa wananchi wake.
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega amemaliza ziara hiyo kwa kutembelea na kujionea namna teknolojia mbalimbali zinazotumiwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Bahari Kuu Zanzibar katika uhifadhi wa Bahari ya Hindi pamoja na kupata taarifa sahihi za shughuli za uvuvi zinazofanywa baharini katika eneo la Tanzania.