Home Michezo Kuelekea Mechi ya Watani wa Jadi…SIMBA Wamelishwa Nini?

Kuelekea Mechi ya Watani wa Jadi…SIMBA Wamelishwa Nini?

19
0
SIMBA wamelishwa nini? Hilo linaweza kuwa swali sahihi kwa mashabiki, wanachama na viongozi wa timu hiyo kutokana na mzuka walionao kuelekea pambano la kukata na shoka dhidi ya watani wao wa jadi, Yanga.
Japo katika soka kuna matokeo ya aina tatu, yaani ushindi, sare na kufungwa, lakini watu wa Simba wamekuwa na uhakika wa asilimia 100 wa kuwafunga Yanga Jumamosi katika mchezo wa marudiano wa Ligi Kuu Tanzania Bara, utakaopigwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Japo Simba wanafahamu kuwa Yanga ndio mabingwa watetezi wa ligi hiyo ambao wameonekana kuwa ngangari, wakiwa wamepigwa tafu na ushiriki wao wa mashindano ya kimataifa, lakini kwa Wekundu wa Msimbazi hao, hayo hayawasumbui kichwa wakiamini ‘Yeboyebo’ lazima ikatike siku hiyo.
Kinachowapa jeuri Simba, si kama wamenyweshwa ‘kizizi’ au vinginevyo, bali ni kutokana na imani ya ubora wa kikosi chao kinachoundwa na wachezaji wenye uwezo wa kiwango cha juu, hasa wale wanaounda safu ya kiungo.
Lakini pia, safu ya ulinzi inayoongozwa na Method Mwanjali na ile ya ushambuliaji ‘iliyofufuka’ baada ya Laudit Mavugo na Ibrahim Ajib kuunda upacha wa aina yake, wakitarajiwa kushirikiana na fundi Mohammed Ibrahim ‘Mo’, ndivyo vinavyowapa kichwa watu wa Simba kuelekea ‘Super Saturday’, yaani Jumamosi.
Katika kukoleza hayo, Simba imeweka mikakati kabambe ikiwamo Rais wao, Evans Aveva, kukutana na viongozi na wanachama wa matawi yao yote ya Dar es Salaam kujipanga kuhakikisha Yanga hatoki siku hiyo.
Katika kikao hicho kilichofanyika Ijumaa iliyopita, pamoja na mambo mengine walijadili juu ya pambano la Jumamosi dhidi ya Yanga, lakini pia mbio za ubingwa.
Tayari Simba wameweka kambi visiwani Zanzibar, lakini kukiwa na usiri mkubwa wa nini kinaendelea huko.
Meneja wa Simba, Mussa Hassan ‘Mgosi’ ambaye kwenye kurasa zake mbalimbali za mitandao ya kijamii amekuwa akiandika ujumbe tata kama ‘Walete Walete Watufungulie Njia za Ubingwa,’ amedai kuwa mechi yao na Yanga ni kama mechi nyingine tu.
“Ni muhimu kwetu sana kwa sababu tukishinda hapa, mbio za ubingwa zinazidi kukolea lakini kila mpinzani wetu tunampa uzito mkubwa ila ushindi kwetu utatusaidia kurejea kuongoza,” alisema.
Simba wapo kileleni mwa msimamo wakiwa na pointi 51 katika michezo 22 waliokwishakucheza mpaka sasa, huku Yanga wakiwa nafasi ya pili na pointi 49 wakicheza michezo 21 ambapo timu itakayoshinda itakuwa na nafasi nzuri ya kusimama kileleni.