Home Michezo MAN UTD KUAMUA HATMA YA MICHAEL CARRICK

MAN UTD KUAMUA HATMA YA MICHAEL CARRICK

59
0

Kiungo Michael Carrick ameahidi kustaafu soka, endapo uongozi wa Man Utd utasitisha mpango wa kumsainisha mkataba mpya mwishoni mwa msimu huu.

Carrick mwenye umri wa miaka 35, amekua Old Trafford tangu Julai 2006 akitokea Tottenham Hostspurs, na mkataba wake utafikia kikomo mwezi Juni mwaka huu.

Carrick ambaye tayari ameshacheza michezo 22 akiwa na Man Utd msimu huu, amesema hana mpango wa kujiunga na klabu nyingine, na kama itashindikana kusaini mkataba mpya atajiweka pembeni.

Amesema mazungumzo ya kusaini mkataba mpya wa kuendelea kucheza soka klabuni hapo kwa sasa yamesitishwa kwa muda, lakini anaamini kabla ya msimu huu kufikia kikomo atakua ameshafahamu mustakabali wake.

“Sina papara ya kutaka kujua nitasaini ama sitosaini mkataba mpya, jambo hili ninaawachia viongozi wangu, lakini ikitokea suala la kutosaini mkataba mpya linapewa nafasi, nitaaamua kustaafu soka.” Alisema Carrick alipozungumza na shirika la utangazaji la Uingereza BBC.

Carrick ni mchezaji aliyedumu kwa muda mrefu klabuni hapo kwa sasa, akitanguliwa na mshambuliaji Wayne Rooney, na tayari ameshacheza michezo 400 huku akitwaa ubingwa wa England mara tano, ligi ya mabingwa Ulaya mara moja, kombe la FA na kombe la ligi mara tatu.