Home News MCHANGE AWAITA AKINA ZITTO MAJUHA KWA KUPINGA MUSWADA SHERIA VYAMA VYA SIASA...

MCHANGE AWAITA AKINA ZITTO MAJUHA KWA KUPINGA MUSWADA SHERIA VYAMA VYA SIASA MAHAKAMANI

1723
0

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

TAASISI ya Vugu Vugu la Mendeleo nchini imeunga mkono Muswada wa Mabadiliko ya Sharia ya Vyama vya Siasa, huku ikiwaita majuha wanasiasa waliofungua shauri la kuupinga muswada huo kwenye Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam.

Itakumbukwa ni muda sasa vyama vya siasa vya upinzani vimekuwa vikiupinga muswada huo na moja ya sababu viyotaja ni kwamba unakwenda kumpa madaraka makubwa Msajili wa Vyama vya Siasa ya kuwa na uwezo wa kuingilia maamuzi ya vyama hivyo.

Kutokana na hali hiyo vyama vya upinzani kupitia Kiongozi wa Chama cha ACT- Wanzalendo Zitto Kabwe na wenzake walitangaza kufungua shauri hilo mahakamani la kuupinga kujadiliwa bungeni ambapo Januari 4, 2019 shauri lilianza kusikilizwa.

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo Habib Mchange alisema wanaunga mkono msawada huo kwani unakwenda kuwa na majibu ya namna ya kudhubiti matumizi ya fedha za ruzuku pamoja na wanachama kupata mahali pa kupeleka malalamiko yao.

“Mimi na Asasi yangu na vijana wenzangu tunasema huyu aliyeamua kupeleka muswada huu amefanya jambo sahihi na kwa wakati sahihi, wanasiasa waliokwenda kupinga muswada huu mahakamani ili usijadiliwe bungeni ni Majuha,” alisema Mchange.

Aidha aliongeza kwa kutaja faida za muswada huo kuwa utakwenda kusaidia katika utatuzi wa migogoro inayotokea ndani ya vyama kwani wanachama watapata mahali pa kupeleka malalamiko yao pamoja na kuondoa Umungu mtu katika vyama.

Akifafanua juu ya Umungu mtu ndani ya vyama alisema ni kutokana na kutokuwepo kwa mfumo mzuri katika vyama unaoonesha ukomo wa madaraka hali inayofanya viongozi kwenye nafasi fulani ndani ya vyama kuwa wakudumu.

Alieleza kuwa muswada huo utakwenda kuweka mfumo mzuri wa upatikanaji wa viongozi katika vyama pamoja na kuvifanya kuweka vipengele vya ukomo wa viongozi wake.

“Hakuna mfumo mzuri wa upatikanaji wa viongozi ndani ya vyama, vyama vinamilikiwa na watu, na vipengele vya ukomo wa madaraka vimenyofolewa (Chadema),” alibainisha Mchange.

Mchange alitoa wito kwa Watanzania kusaidia kufanikisha kukamilika kwa sheria hiyo kwa kusisitiza kuwa itakwenda kuondoa Umungu Mtu pamoja na kusimamia vizuri matumizi ya fedha za ruzuku kwani ni kodi zao hivyo wanahaki yakujua jinsi inavyotumika.

Muswada huo wa Mabadiliko ya Vyama vya Siasa unatarajiwa kujadiliwa kwenye mkutano wa kumi na nne wa Bunge lijalo la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.