Home News MKATABA WA MAKUBALIANO YA PARIS KUIWEKA SALAMA TANZANIA

MKATABA WA MAKUBALIANO YA PARIS KUIWEKA SALAMA TANZANIA

1371
0
Na Ismail Ngayonga,MAELEZO,DAR ES SALAAM
MABADILIKO ya tabia nchi ni mabadiliko ya mtiririko wa mfumo wa hali ya hewa yanayochukua muda mrefu au mfupi na kusababisha hali mbaya za hewa ama uchache wa hali inayohitajika na kusababsisha madhara.
Inaelezwa kuwa kwa kiasi kubwa, mabadiliko ya hali ya hewa yanasabishwa na shughuli za kibinadamu ikiwemo shughuli za viwanda, ambapo takwimu zinaonesha kuwa tani billion 9 za hewa ya ukaa zinatolewa angani kila siku kutokana na shughuli za viwanda.
Athari za mabadiliko ya tabianchi zinatishia sana maisha ya watu wengi duniani, ambapo nchi mbalimbali za Bara la Afrika ikiwemo Tanzania zinazoendelea na zimekuwa na mwamko mkubwa kuhusu suala la mabadiliko ya tabianchi kutoka na athari na changamaoto zinazowakabili katika ngazi mbalimbali.
Athari za mabadiliko ya tabianchi ni pamoja na kuongezeka kwa usawa wa bahari kutokana na kuyeyuka kwa barafu katika Bahari ya Arctic na Antactica, kuongezeka kwa matukio ya vimbunga, kupungua kwa kasi kubwa kwa kiwango cha theluji katika vilele vya milima, ukame wa mara kwa mara unaosababisha upungufu wa maji, chakula na nishati ya umeme.
Aidha madhara mengine ni pamoja kuenea kwa magonjwa kama vile malaria katika maeneo ambayo haukuwa wa kawaida; na mmomonyoko wa ukanda wa bahari unaotishia uharibifu wa miundombinu iliyopo katika maeneo hayo.
Katika kubaliana na changamoto hiyo, Jumuiya ya Kimataifa inashikamana kwa dhati ili kudhibiti athari za mabadiliko ya tabianchi kwa kutekeleza kwa vitendo makubaliano ya Mkutano wa 21 wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mkataba wa Mabadiliko ya Tabianchi uliofanyika mjini Paris, nchini Ufaransa, kuanzia tarehe 30 Novemba hadi 12 Desemba 2015.
kwa kuzingatia manufaa yatokanayo na Mkataba huo pamoja na itifaki yake kwa Tanzania na umuhimu na manufaa ya makubaliano hayo, Bunge katika Mkutano wake wa Kumi na Moja na kwa mujibu wa Ibara ya 63 (3)(e) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, liliazimia kuridhia makubaliano hayo.
Akiwasilisha Hotuba ya Makadirio ya Bajeti na Matumizi kwa mwaka 2018/19, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), January Makamba anasema katika kipindi cha mwaka wa fedha 2017/18, Serikali iliendelea  kuratibu  utekelezaji wa miradi miwili ya kuhimili mabadiliko ya tabianchi iliyo chini ya Mkataba wa Makubaliano ya Paris.
Anasema miradi hiyo ni pamoja na mradi  wa kujenga uwezo wa jamii za Pwani kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi na mradi wa kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi katika Jiji la Dar es Salaam.
Waziri Makamba anasema kupitia mradi wa Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi katika Jiji la Dar es Salaam, Serikali imekamilisha ujenzi wa ukuta wa fukwe wa bahari wenye urefu wa mita 920 katika Barabara ya Obama na ukuta wa bahari wenye urefu wa mita 500 katika Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere.
“huduma muhimu kama vile vyoo, taa za usalama na sehemu za kupumzikia zimewekwa katika eneo la mradi sambamba na ujenzi wa mitaro mitaro/ mifereji ya maji ya mvua yenye urefu wa mita 475 katika maeneo ya Bungoni, Manispaa ya Ilala na mifereji ya maji ya mvua yenye urefu wa mita 550 katika Manispaa ya Temeke” anasema Waziri Makamba.
Akifafanua zaidi Waziri anasema katika Mradi  wa  Kujenga Uwezo wa Jamii za Pwani Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi, Serikali imekamilika ujenzi wa ukuta wa mita 600 katika ufukwe wa Pangani Tanga na ukuta wa mita 50 katika ufukwe wa Kisiwa Panza, Pemba pamoja na kuweka makinga mawimbi katika eneo la Kilimani-Unguja.
Aidha Makamba anasema Serikali pia imefanikisha zoezi la upandaji wa mikoko katika wilaya ya Rufiji (hekta 792), wilaya ya Pangani (hekta 10) na Zanzibar (hekta 235) pamoja na uchimbaji wa visima 10 na ujenzi wa miundombinu ya kuvuna maji ya mvua katika shule za Sekondari Kingani na Matipwiri, Bagamoyo, Mkoani Pwani.
Anaongeza kuwa katika mwaka 2017/18, Ofisi yake iliendelea  na  mchakato  wa  kuwezesha  sekta  za umma na binafsi hapa nchini kupata ithibati katika Mfuko wa Mabadiliko ya Tabianchi na kujenga uwezo kwa taasisi kupata fedha za kutekeleza miradi ya mazingira kutoka mifuko mbalimbali ya mazingira duniani.
Kwa mujibu wa Waziri Makamba anasema katika mwaka wa fedha wa 2018/19, Ofisi yake inatarajia kuendelea kutekeza miradi mingine chini ya Mkataba wa Mabadiliko ya Tabianchi ikiwemo Mradi wa Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi katika maeneo ya Vijijini kupitia Mfumo Ikolojia katika maeneo  ya Kishapu, Mpwapwa, Mvomero, Simanjiro na Kaskazini A Unguja.
Kwa mujibu wa Waziri Makamba anasema, katika mwaka wa fedha 2018/19, Serikali itaendelea kuratibu uchambuzi wa miradi chini ya ufadhili wa Mfuko  wa  Mabadiliko  ya  Tabianchi  na kuhamasisha sekta binafsi, taasisi za umma na mashirika ya kitaifa kuandaa miradi  ya  mabadiliko  ya tabianchi.
Ni wajibu wa jamii, Serikali na taasisi zake, mashiŕika ya kiraia na mtu mmoja mmoja kufanya kazi ya kuhakikisha kuwa mipango yoyote ya maendeleo inahusisha pia kujikinga na mabadiliko ya tabia nchi kama suala mtambuka.