Home News MWINGIRA WA EFATHA ADAI KUWEPO MAKUNDI MATATU YAKUMWANGAMIZA MAKONDA

MWINGIRA WA EFATHA ADAI KUWEPO MAKUNDI MATATU YAKUMWANGAMIZA MAKONDA

1551
0

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

MTUME na Nabii wa Kanisa la Efatha Ministry Josephat Mwingira, amedai kuwepo kwa makundi makubwa matatu ambayo yamejipanga kumuangamiza Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda.

Mwingira alisema hayo leo kanisani kwake jijini Dar es Salaam katika Ibada ya Jumapili ambayo ilihudhuriwa na Mkuu huyo wa Mkoa ikiwa na lengo la kukemea vitendo vya ushoga jijini hapa.

“Yapo makundi makubwa matatu yamejipanga kukuangamiza na tena yana nguvu kubwa sana,” Mwingira alimwambia mkuu wa mkoa Makonda.

Mtume na Nabii huyo alimuombea Makonda ili kuwa na ulinzi wa Mungu kwa ajili ya kumkinga dhidi ya makundi hayo ili aendelee kuwatumikia wananchi.

Alimtia moyo katika kampeni yake ya kupambana na vitendo vya ushoga ambapo alimsihi kutokata tamaa kwa kuwa kazi anayofanya ni njema mbele za Mungu.

Aidha Mwingira alisema kuwa kwa sasa hofu ya Mungu imeanza kupotea  na hivyo kusababisha maadili kuporomoka nchini.

Aliongeza kuwa Tanzania inapitia katika kipindi kigumu lakini akaeleza kuwa Mungu anajua inapokwanda na itafanikiwa kufika salama huku akibainisha kwamba kipindi cha nyuma waovu walikuwa wakionekana wajanja tofauti na hivi sasa.

Kwa upande wa mkuu wa mkoa Paul Makonda akizungumza wakati wa ibada hiyo alieleza kuwa amekuwa akikabiliana na changamoto mbali mbali katika utumishi wake kama mkuu wa mkoa.

Alisema pamoja na changamoto hizo amekuwa akimtumikia Mungu kwa njia tofauti tofauti kama kiongozi kutokana na kwamba anatakiwa kuwa mfano ndiyo maana amekuwa akipambana na mambo kama ya dawa za kulevya.

Alitoa wito kwa wa umini wa kanisa hilo kuendelea kumtumikia Mungu kwani yeye ndiye anayewapa uwezo na nguvu ya kuwasaidia hapa duniani na kwa ajili ya kupata uzima wa milele.

“Kile ambacho mtumishi anafundisha muamini kua kweli Mungu anatenda, hadi leo hii mimi kama siyo Kristo nisingekuwa hapa,” alisema Makonda.

Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa Mkoa akiwa katika kanisa la Victoria Christian Center aliwataka wazazi kukaa na kutoa elimu kwa watoto wao ili kuwaepusha kujiingiza katika vitendo vya ushoga. 

Aidha alisema kuwa kuanzia kesho itaanza operesheni kali ya kupambana na mashoga, wasagaji, biashara ya ngono na matapeli wa njia ya mitandao. 
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda akiombewa na Mtume na Nabii wa Kanisa la Efatha Ministry jijini Dar es Salaam.