Home News NAIBU WAZIRI OLE NASHA ASEMA SOMO LA HISABATI NDIYO NGUZO KUELEKEA UCHUMI...

NAIBU WAZIRI OLE NASHA ASEMA SOMO LA HISABATI NDIYO NGUZO KUELEKEA UCHUMI WA VIWANDA

1731
0

Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. William Ole Nasha amesema kuwa ili nchi iweze kupiga hatua Katika  uchumi wa viwanda lazima nguvu kazi na msisitizo uelekezwe kwenye masomo ya Sayansi ikiwemo  somo la hisabati.

Mhe. Ole Nasha amesema  hayo Wilayani Korogwe, mkoani Tanga wakati akifunga mafunzo ya hisabati kwa walimu ambao mikoa yao imekuwa haifanyi vizuri katika somo hilo.

“ Hisabati inaonekan ni kitu kigumu hivyo walio wengi wamekuwa na hofu, ukweli ni Kwamba hisabati ni maisha, hisabati ni kujua una ng’ombe wangapi? Unapandaje mbegu zako shambani, hivyo walimu wanaofundisha somo la hisabati lazima wabadilike kwa kuwa na mbinu ambazo zitawasaidia wanafunzi wasione kuwa somo hilo ni gumu ili waweze kufanya vizuri,” alisisitiza Ole Nasha.

Amesema kuwa Mwalimu mzuri ni yule anayemsaidia mwanafunzi kufaulu na siyo vinginevyo  na kusisitiza kuwa kitu rahisi katika   maisha ya kila siku ya mwanadamu ni hisabati, kwa kuwa kila jambo ambalo linafanyika linahitaji mipango na hiyo ni hisabati.

Naibu Waziri pia alitumia hadhira hiyo kuelezea baadhi ya mafanikio yaliyopatikana katika sekta ya Elimu katika miaka Mitatu ya uongozi wa Mhe. Rais John Magufuli kuwa ni pamoja na kuongezeka kwa idadi ya uandikishaji wa wanafunzi wanaojiunga na Elimu msingi kutokana na Elimu bila malipo ambapo kila mwezi serikali inatuma kwenye shule kiasi Cha zaidi ya bilioni 23.

Mengine ni  Wizara kujenga Shule 500,
Uboreshaji wa vyuo va Ualimu, uboreshaji wa mitaala, ukarabati wa shule kongwe,usambazaji wa vifaa vya maabara, usambazaji wa vifaa vya wanafunzi wenye mahitaji maaluu kwa nchi nzima, kuongezeka kwa idadi ya wanafunzi ni wanufaika wa mikopo ya Elimu ya Juu.

Nao washiriki wa mafunzo hayo kupitia risala yao wamemhakikishia Naibu Waziri kuwa mafunzo na mbinu walizozipata katika kufundisha somo la  hisabati watahakikisha Matokeo ya somo hilo sasa yanaenda kuwa Chanya.

Mafunzo hayo  ya siku 7 yameratibiwa na Idara ya Elimu ya Ualimu kupitia mradi wa kuendeleza Elimu ya Ualimu (TESP) yameshirikisha maeneo ya Mkalama, Simanjiro, Meatu, Gairo, Ruangwa, Nanyamba, Rufiji, Nyasa, Momba, Korogwe, Ukerewe,  na Madaba.

Imetolewa na;
Kitengo Cha Mawasiliano Serikalini
WIZARA YA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA
22/12/2018