Home Uncategorized NEC YAKANUSHA TUHUMA ZA CHADEMA

NEC YAKANUSHA TUHUMA ZA CHADEMA

2512
0
……………………..
Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Dkt. Athumani Kihamia akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam leo (Alhamisi 20.09.2019). Dkt. Kihamia amekanusha tuhuma zilizotolewa na Mwenyekiti wa Chadema, Mhe. Freeman Mbowe kwenye mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika jana (Jumatano 19.09.2019). (Picha na NEC)
Na. Idara ya Habari-NEC
Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Dkt. Athumani Kihamia amekanusha Tuhuma zilizotolewa na Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Mhe. Freeman Mbowe dhidi ya Tume kutokana na uchaguzi Mdogo wa Jimbo la Monduli na Ukonga.
Uchaguzi mdogo katika Jimbo la Monduli, Mkaoni Arusha na Ukonga Jijini Dar es Salaam ulifanyika Tarehe 16, Septemba mwaka huu pamoja na Kata 23 za Tanzania Bara.
Dkt. Kihamia akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam leo (20.09.2019) amesema tuhuma zilizotolewa na Mbowe dhidi ya Tume na dhidi yake binafsi hazina ukweli wowote.
Dkt. Kihamia aliwathibitishia waandishi wa habari kwamba tuhuma kwamba kulikuwa na vituo ‘fake’ 16 kwenye uchaguzi mdogo wa Jimbo la Ukonga ni za uongo na kwamba vituo vilivyotumika ni 673 ambavyo ni vilevile vilivyotumika kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.
“Vituo vilevile 673 vilivyotumika kwenye Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2015 ndio hivyohivyo vilivyotumika kwenye uchaguzi mdogo wa Septemba 16 Jimbo la Ukonga. Hakujapunguzwa kituo hata kimoja wala kuongozwa kituo hata kimoja…,” alisema.
Dkt. Kihamia aliongeza kwamba wakala wa Chadema wa kujumlisha matoke, Bi. Asia Msangi ambaye pia alikuwa mgombea wa chama hicho Jimbo la Ukonga alisaini fomu ya matokeo jambo ambalo linaonyesha kwamba chama hicho kiliridhia mchakato huo.
Mkurugenzi huyo wa Uchaguzi alisisitiza kwamba ni vyema chama hicho kikawaeleza wananchi ukweli juu ya sababu zilizowapelekea kushindwa kwenye chaguzi hizo badala ya kuizushia Tume uongo kila mara.
“Watanzania wasipotoshwe, wanasiasa wasitafute sababu za kushindwa kwa kuzungumza mambo yasiyokuwa na ukweli na kama tuhumu za Chadema ni za ukweli basi ni bora wakaenda mahakamani. Hizi ni tuhuma za uongo zenye lengo la kujiosha,” alisema.
Kuhusu Monduli na tuhuma kwamba kuna mawakala wa Chadema waliozuiliwa, Dkt. Kihamia amesema kwamba wapo watu wasiokuwa mawakala wanaotambulika kisheria walitaka kukiwakilisha chama hicho na hivyo walizuiliwa.
“Sio kweli kwamba mawakala walikataliwa na kutolewa nje ila kilichotokea ni kwamba wapo watu ambao walifika kituoni kwenye vituo vinne tofauti wakidai kwamba ni mawakala wakati hawajaapa kufanya kazi hiyo kwa hiyo watu kama hao hawawezi kuruhusiwa,” alisema.
Mkurugenzi aliongeza kuwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi iliwatuma Makamishna na Maofisa wake kwenye maeneo yote ambayo yalikuwa yanafanya uchaguzi ili kufuatilia mwenendo wa uchaguzi kwa hiyo Tume ina taarifa za uhakika juu ya yale yote yaliyojiri.
Kuhusiana na kujitokeza kwa wapiga kura wachache, Dkt. Kihamia alisema kwamba kwa kawaida chaguzi ndogo huwa hazina msisimko mkubwa kwa wapiga kura kwa hiyo idadi ya wapiga kura waliojitokeza sio ya kushangaza.
“Ukifanya utafiti duniani kote utagundua kwamba chaguzi ndogo huwa hazina wapiga kura wengi, kwa hiyo hili sio jambo la kushangaza,” alisema.
Katika hatua nyingine, Dkt. Kihamia alimtaka, Mhe. Mbowe kumuomba radhi kwa kumtuhumu kuwa yeye ndio anahusika na mambo yaliyokinyume na sheria ndani ya Tume.
“Mhe. Mbowe sijawahi kukutana naye na yeye hajawahi kukutana na mimi, kwa maana hivyo hatujawahi kugombana, hivyo anatakiwa achague maneno ya kusema…..mimi sipendi kulumbana na wanasiasa na wanasiasa wengine wote waelewe hivyo, nipo hapa kuhakikisha kwamba Tume inatimiza wajibu wake,” alisema.