Ngoma, Tambwe waipania Azam - The Choice

Ngoma, Tambwe waipania Azam

0
DONALDO NGOMA.

WASHAMBULIAJI Donald Ngoma na Amissi Tambwe ambao walikuwa majeruhi na kukosa mchezo wa marudiano dhidi ya Zanaco, wameanza mazoezi na sasa wanaelekeza akili yao kwenye mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Azam FC.

Yanga itaumana na Azam Aprili Mosi, mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa.

Ngoma na Tambwe waliliambia Nipashe kwa nyakati tofauti kuwa, wanapambana kujiweka fiti ili kuanza kuitumikia timu hiyo kwenye mchezo dhidi ya Azam FC.

Ngoma, alienda mbali na kusema ameumia kuona timu yake imetolewa kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na sasa wanataka kuelekeza nguvu yao kwenye mchezo dhidi ya Azam ili kujiweka sehemu nzuri ya kuutetea ubingwa wao.

“Nataka kuwa fiti mpaka kufikia mchezo dhidi ya Azam, tumeondolewa Ligi ya Mabingwa, lakini kabla hatujaanza kuufikiria mchezo wetu wa kwanza wa Kombe la Shirikisho Afrika, tunataka kuanza na Azam kwanza,” alisema Ngoma.

Nyota huyo tegemeo wa Yanga amesema bado wapo kwenye mbio za kutetea ubingwa wao msimu huu na mchezo na Azam utaongeza kasi kufikia nia hiyo.

Alisema wameanza mazoezi mepesi na baada ya muda mfupi wataungana na wachezaji wenzao kwenye program ya kocha wao, George Lwandamina.

Facebook Comments
Share.

About Author