Nini kinaiua Ndanda FC - The Choice

Nini kinaiua Ndanda FC

0

Na Makoleko Kalibonge II

HAKUNA timu inayopeanda kushuka daraja. Ni kwa sababu ya utaratibu tu uliowekwa kulingana na matakwa ya ligi husika kuwa, ligi itakuwa na timu kadhaa kwa msimu na timu kadhaa za chini kabisa zitashuka daraja na kadhaa zitapanda kuchukua nafasi yazo, na timu moja itakuwa bingwa na mambo mfano wa hayo.

Ni kutokana pia na kuimarisha soka la nchi hata ukawekwa utaratibu huo. Haishindikani ligi kushirikisha timu zote bali ni kwa sababu lazima kuhakikisha ushindani unawepo. Na hapo ndipo huja idadi maalumu ya timu kwenye ligi na idadi ya timu za kushuka na kupanda daraja.

Kadhalika, hakuna wachezaji wanaopenda kuwa na sifa ya kushindwa kuinusuru timu wanayoichezea isishuke daraja. Kwa hivi wanafahamu kuwa ni aibu katika maisha yao ya soka. Ni sifa mbaya kubainishwa kwa mchezaji kwa namna ambayo imeifanya timu fulani kushuka daraja. Ndiyo maana wachezaji hujituma katika mazingira ambayo ni kutokana na utaratibu wa ligi ndiyo huwafanya waishie njiani.

Wachezaji wanafahamu fedheha ya kuishusha timu daraja kwa sababu huwa kazi kubwa sana kuaminiwa katika timu nyingine – ni aibu kwao.

Pia, viongozi nao hufadhaika sana timu yao inaposhuka daraja. Maana yake ni kwamba, wanakosa sifa ya kuwa viongozi. Wameshindwa kuisimamia timu ikafanya vizuri na kuendelea kushiriki ligi. Lakini wakati mwingine, mbali na taratibu za ligi husika, pia jitihada hazishindi kudra.

Aidha, anayeathirika sana kwa timu kushuka daraja ni mwalimu (kocha) wa timu. Mwalimu huathirika kwa sababu huandamwa sana na mzimu wa mashabiki. Ndiyo maana kuna wakati timu humfukuza mwalimu kutokana na timu hiyo kufanya vibaya – kutopata matokeo yanayoridhisha.

Mwalimu huandamwa na mzimu wa mashabiki kwa fikra kuwa hakuwa na mbinu za kiufundi kuisaidia timu. Upeo wake wa kuwajenga wachezaji kisaikolojia katika kila unapowadia wakati wa kucheza na timu nyingine. Ameshindwa kukiaminisha kikosi chake kuwa kinaweza kupambana na kupata matokeo mazuri ya kuwafanya mashabiki kufurahia uwepo wa timu hiyo.

Ni kitu gani kinasababisha Ndanda FC ya Mtwara ifanye vibaya kwenye Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara? Ndilo swali ninalojiuliza kila wakati hasa tangu kuanza kwa mzunguko wa pili wa ligi hiyo.

Mechi tano mfululizo tangu mzunguko wa pili umeanza, Ndanda FC haijafanikiwa kushinda hata moja. Na, siyo haijafanikiwa kushinda tu, bali haijapata hata sare. Na zaidi ni kwamba katika mechi hizo haijafunga hata bao moja la kufutia machozi. Maana yake ni kuwa, imepoteza pointi 15 ambazo ni nyingi sana kwa timu kama Ndanda FC ambayo imekuwa katika wakati mgumu sana.

Tangu mzunguko wa pili umeanza timu hiyo imecheza mechi tano; mechi tatu nyumbani na mbili ugenini. Ilianza kufungwa na Simba SC mabao 2-0 katika mchezo wa kwanza uliopigwa uwanja wa Nangwanda Sijaona, kisha ikafungwa na Mtibwa Sugar mabao 2-0 katika uwanja huo huo.

Baadaye ikachapwa na Yanga SC mabao 4-0 katika mchezo wa tatu uliopigwa uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam kabla ya kufungwa mabao 2-0 na Kagera Sugar katika mchezo uliopigwa uwanja wa Kaitaba na mechi ya tano wamekubali kulala kwa bao 1-0 kutoka kwa Majimaji FC katika uwanja wa Nangwanda Sijaona.

Ni wakati mgumu sana kuwahi kutokea katika timu ya Ndanda F.C. Kwa matokeo hayo sasa timu hiyo inaangukia kwenye timu tatu za mkiani wakizidiwa pointi moja na Majimaji FC.

Mchezo unaofuata timu hiyo itasafiri kuifuata Azam FC katika mchezo utakaopigwa uwanja wa Azam Complex jijini Dar es Salaam. Hatuwezi kuikatia tamaa katika mchezo huo, lakini kwa mwenendo huu ni wazi utakuwa mchezo mgumu zaidi kwa Ndanda FC.

Ni nini hasa kipo nyuma ya matokeo mabovu ya Ndanda F.C? Wachezaji hawajitumi, uongozi haufahamu majukumu yake au mwalimu ameishiwa mbinu?

Ni fedhea sana kuliona jahazi la Ndanda FC likizidi kwenda mrama. Ndanda FC ambayo kupanda kwake daraja kuliamsha ari na morali kwa wapenda soka mkoani Mtwara wakiamini wamepata timu baada ya kusota miaka 10 bila kuwa na mwakilishi wa soka lao katika Ligi Kuu Tanzania Bara.

Hadi kufikia raundi ya 20 Ndanda FC haijakusanya pointi za kutosha – imekusanya pointi 19 katika mechi 20 wastani wa pointi 0.95 kwa kila mchezo. Ni hali mbaya sana na itakuwa na safari ndefu sana ya kutembea kuhakikisha inakusanya pointi za kutosha katika mechi 10 zilizobaki ili kujihakikishia kucheza Ligi Kuu Tanzania Bara msimu ujao.

Kwa matokeo haya mabaya, ni budi wachezaji, viongozi na benchi la ufundi liwajibike kwa namna yoyote. Kama kuna tatizo liwekwe wazi kwa namna yoyote iwayo ili pengine litatuliwe na kuinusuru timu kwa mwenendo huu, vinginevyo hakuna salama kwa timu hiyo kurejea Ligi Daraja la Kwanza.

Kama ni wachezaji wafahamu kuwa kushuka daraja kwa Ndanda kutawafanya wapotee Ligi Kuu na ndoto zao katika maisha ya soka zitapotea. Kama ni viongozi nao watambue hawatokuwa na sifa ya uongozi wa soka ikiwa timu hii itashuka daraja kwa sababu watakuwa wameshindwa kujidhihirisha uwezo na weledi wao katika kuongoza timu.

Kadhalika, kama ni benchi la ufundi, basi watambue kuwa kushuka daraja kwa Ndanda kutathibitisha uwezo wao mdogo waliokuwa nao katika kuwaandaa wachezaji. Kama wadau wa soka nao watafutiwe mwarobaini wao.

Bali lawama hazitoenda kwa yeyote iwapo tu atawekwa wazi ‘mchawi’ wa timu kufanya vibaya bila kujali ama nafasi au hadhi aliyokuwa nayo. Tunataka kuiona Ndanda FC ikicheza Ligi Kuu msimu ujao. Mechi 10 zinatosha sana kwa timu hiyo kusalia kwenye Ligi Kuu ingawaje zinatosha pia kuipoteza timu hiyo kwenye ligi hiyo.

Share.

About Author