Okwi Afumuwa Kikosi cha Simba Leo

0

UJIO wa mshambuliaji wa Simba, Mganda, Emmanuel Okwi, umemfanya kocha msaidizi wa timu hiyo, Mrundi, Masoud Djuma kufumua kikosi chake cha leo kitakachoivaa Kagera Sugar.

Hiyo, ni baada ya mshambuliaji huyo kurejea nchini na kucheza mechi dhidi ya Singida United akitokea benchi, akichukua nafasi ya James Kotei na kufunga mabao mawili kwenye ushindi wa mabao 4-0.

Simba inatarajiwa kuvaana na Kagera leo katika mechi ya Ligi Kuu Bara itakayochezwa kwenye Uwanja wa Kaitaba huko Kagera.

 

Akizungumza na Championi Jumatatu, Djuma alisema kuwa amevutiwa na kiwango cha Okwi alichokionyesha huku akicheza kwa maelekezo yake, hivyo upo uwezekano mkubwa wa mshambuliaji huyo kumuondoa mchezaji mmoja katika kikosi cha kwanza ili yeye aingie kikosini.

 

Djuma alisema, Okwi anafaa kwenye mfumo wake kutokana na aina yake ya uchezaji wa soka la mashambulizi ya kushtukiza ‘counter attack’ wakiwa wanashambulia goli la wapinzani wakati wakiwa na mpira.

Djuma alisema, anafurahia kuona Okwi akijiunga na timu na kuushika haraka mfumo wake wa kushambulia goli la wapinzani wakiutumia mfumo ambao awali ulikuwa unabezwa wa 3-5-2 na kupata matokeo mazuri ya ushindi wa mabao mengi.

 

“Nikuhakikishie kuwa, kama Okwi akiendelea kufanya mazoezi kwa muda mrefu na timu na kuushika mfumo wangu huu mpya vizuri zaidi ya hivi sasa, basi nikuhakikishie timu yangu itapata matokeo mazuri katika michezo ijayo ya ligi kuu.

“Ninakwenda kucheza na Kagera, huenda kikosi changu kikawa na mabadiliko kidogo, ni baada ya Okwi kuingia kwenye mfumo wangu vizuri na kuushika, hivyo upo uwezekano wa mchezaji mmoja kumpisha Okwi,” alisema Djuma.

 

2,478 total views, 6 views today

Facebook Comments
Share.

About Author