Home Michezo PAUL STRETFORD AMPIGANIA ROONEY, AELEKEA MASHARIKI YA MBALI

PAUL STRETFORD AMPIGANIA ROONEY, AELEKEA MASHARIKI YA MBALI

13
0

Wakala wa mshambuliaji wa Man Utd Wayne Rooney ameripotiwa kuelekea nchini China kwa ajili yakufanya mazungumzo na baadhi ya klabu za ligi kuu ya soka nchini humo, ili kuangalia uwezekano wa kumuhamisha mchezaji wake kabla ya dirisha la usajili halijafungwa.

Harakati za usajili nchini China zinatarajiwa kufungwa mwishoni mwa mwezi huu (Siku ya jumanne), na tayari kuna tetesi ambazo zinadai kuna uwezekano mkubwa Rooney akaondoka Old Trafford.

Paul Stretford wakala wa mshambuliaji huyo kutoka nchini England, amekua mmoja wa wanaochukizwa na maisha ya Rooney katika kipindi hiki, ambapo hapati nafasi ya kucheza kwenye kikosi cha kwanza mara kwa mara.

Hata hivyo bado haijafahamika Stretford anafanya mazungumzo na klabu gani za China, lakini baadhi ya vyombo vya habari vimesisitiza safari yake ya kuelekea mashariki ya mbali huenda ikawa na jambo kabla ya dirisha la usajili kufungwa siku ya jumanne.

Meneja wa Man Utd Jose Mourinho alipoulizwa na waandishi wa habari kuhusu uwezekano wa mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 31 kuondoka, alijibu hana uhakika na jambo hilo zaidi ya kutambua Rooney ni sehemu ya kikosi chake.