Home News SAMIA AAHIDI KERO ZA WAKAZI WA PANDE /BAGAMOYO WANAOPISHA MRADI WA BANDARI...

SAMIA AAHIDI KERO ZA WAKAZI WA PANDE /BAGAMOYO WANAOPISHA MRADI WA BANDARI MPYA BAGAMOYO ZITAFANYIWA KAZI

1319
0
NA MWAMVUA MWINYI, PWANI 
WAKAZI wa kijiji cha Pande, wilayani Bagamoyo mkoani Pwani ambao wamehamishwa kupisha mradi wa bandari mpya ya Bagamoyo wameiomba serikali kuwasaidia kulipwa fidia na kuhamishiwa katika makazi mapya .
Akitoa kilio hicho kwa niaba ya wakazi wa maeneo hayo ,wakati makamu wa Rais Samia Suluhu alipokwenda eneo la Mbegani kutembelea ujenzi huo, mwenyekiti wa kitongoji cha Pande Muhsin Mweka alisema  walipangiwa kwenda eneo la Kitopeni na Kidagoni lakini wameshindwa kwenda kutokana fidia kutokamilika.
Alisema kuwa  baadhi ya watu walilipwa fidia lakini wengine hawajalipwa huku wengine wakiwa wamepunjwa fidia zao kwa kulipwa kidogo fedha ambazo hazitoshi kununulia maeneo mengine.
“Wapo waliolipwa hapa hadi laki moja, milioni tano na milioni moja kiasi ambacho hakikidhi, hatujakataa kupisha mradi ila makubaliano yetu hayajatekelezwa “alisema Mweka. 
Kwa upande wake mbunge wa Jimbo la Bagamoyo Dk Shukuru Kawambwa alisema kuwa Kijiji hicho kina kaya 2,200 sawa na watu 16,500 ambao wanatakiwa kuhama eneo hilo.
Kawambwa alieleza, jambo hilo limekuwa ni changamoto kubwa hivyo kuna haja ya kuhakikisha suala hilo linafikia mwisho.
Akijibu hoja hizo,makamu wa Rais  Samia Suluhu alisema , suala hilo amelichukua na atalipeleka kwa Rais baada ya kukaa na mamlaka husika ,wizara ya ardhi, bandari na EPZA ili kulipatia ufumbuzi. 
Samia alifafanua malalamiko yote yatafanyiwa kazi na serikali haitadhulumu mtu haki yake.
Alisema kuhamisha watu hao ni fedha nyingi zinahitajika na kuna taarifa kuwa hata wale walioko eneo la Kitopeni na Kidagoni bado hawalipwa fidia zao .
Alifafanua apewa taarifa awali kuna watu 600 walipatiwa fidia ambazo hazikuwa haki zao ambazo zingesaidia kuwalipa waliostahiki. 
Samia aliwahakikishia serikali kupitia vyombo vyake vya ulinzi na usalama vinafuatilia wahusika hao ili kurejesha fedha hizo. 
Aliitaka halmashauri kuziweka fedha za fidia ya shule na zahanati zinazotolewa eneo hilo bila kutumia kwa matumizi mengine kwani inapaswa nguvu zao zibakie.