Home News SERIKALI YAOMBWA KUTENGA WATAALAMU KUENDESHA VITUO HUDUMA KWA WAHANGA UKATILI WA KIJINSIA

SERIKALI YAOMBWA KUTENGA WATAALAMU KUENDESHA VITUO HUDUMA KWA WAHANGA UKATILI WA KIJINSIA

1055
0

Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dk. John Jingu akikata utepe kuzindua kituo cha kutoa huduma ( One Stop Centre) kilichokabidhiwa na CDF kwa hospitali ya Mwananyamala jijini Dar es Salaam.

Na Abraham Ntambara, Dar es Salaam

SHIRIKA la Jukwaa la Utu wa Mtoto (CDF) limeiomba Serikali kutenga wataalamu wa kutosha wa kuendesha vituo vya huduma kwa wahanga wa ukatili wa kijinsia.

Ombi hilo limetolewa jana jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mtendaji wa CDF Koshuma Mtengeti, wakati shirika hilo likikabidhi kituo cha huduma (One Stop Centre) kwa Hospitali ya Mwananyamala iliyopo Wilaya ya Kinondoni.

“Kituo hiki Kitakuwa kikitoa huduma kwa wahanga wa kesi za ukatili dhidi ya wanawake na watoto lakini na wengineo wote ambao wanakutwa na ukatili wa kijinsia,” alisema Mtengeti.

“Jambo ambalo sisi tunaliomba ni kuona kwamba serikali inatenga wataalamu wa kutosha katika kuendesha vituo hivi, lakini vile vile takwimu ambazo zinatoka katika vituo hivi ni muhimu kuzipata kwani zitasaidia katika kupanga mipango ya baadae ya jinsi gani ya kukabiliana na tatizo hili,” aliongeza.

Mtengeti akitoa ufafanuzi juu ya kituo hicho, alisema kitatoa huduma za kisheria, ushauri nasaha, huduma ya afya pamoja na huduma ya polisi ambao watakuwa wakitoa fomu namba tatu (3) kwa ajili ya matibabu.

Alibainisha kuwa hadi sasa wamekwisha toa mafunzo kwa maafisa 30 ambao watashiriki katika kuendesha kituo hicho pamoja na kufanya mazungumzo na haspitali ya Mwananyamala ili kuona ni jinsi gani ya kushirikiana kwa ajili ya kituo hicho kutoa huduma kwa ufanisi.

Kwa upande wake Afisa Utumishi na Utawala wa Hospitali hiyo Mansour Karama, akizungumza kwa niaba ya Mganga Mkuu alisema wamekuwa wakipokea kwa wingi kesi za ukatili wa kijinsia zinazokumba wanawake, watoto na wanaume.

Karama alisema, kwa wastani wa kesi wanazopokea, asilimia 86 ni ukatili kwa wanawake na asilimia 14 wanaume huku aina za ukatili huo zikiwa asilimia 76 wakingono na asilimia 24 ni wakukataliwa kimwili, kijinsia na kutelekezwa.

Alisema kuwa pamoja na kupokea wahanga hao changamoto kubwa imekuwa ni vitendea kazi pamoja na wahanga kukosa pa kusemea tatizo hilo na kwamba wamekuwa wakiishia kuwapatia matibabu tu. Hivyo alishukuru kukabidhiwa kwa kituo hicho kwani kitakuwa msaada mkubwa katika kutokomeza tatizo hilo.

Naye Katibu MKuu wa Wizara ya Afya, Maedeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. John Jingu alisema kuwa vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto vimekuwa vikiongezeka kwa kasi duniani.

“Ukatili dhidi ya wanawake na watoto ni tatizo kubwa na halikubaliki, hivyo hatua zinatakiwa kuchukuliwa ili kulitokomeza,” alisema Dk. Jingu.

Dk. Jingu alisema kutokana na hali hiyo serikali imekuwa ikifanya jitihada mbali mbali kwa kushirikiana na wadau ikiwa ni pamoja na kuhamasisha uanzishwaji wa vituo hivyo ili kuhakikisha tatizo hilo linakomeshwa nchini.

Aidha aliahidi kuwa serikali itafanya kila liwezekanalo kuhakikisha kituo hicho kinapata kila hitaji ili kiweze kutoa huduma kwa ufanisi.

Chini ya ufadhili wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu Duniani (UNFPA), CDF kwa kushirikana na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, kituo hicho kimekabidhiwa baada ya kukamilisha matengenezo ya kituo pamoja na manunuzi ya vitendea kazi vyake.

Habari picha.