Home News SIDO NGUZO MUHIMU KUELEKEA UCHUMI WA VIWANDA

SIDO NGUZO MUHIMU KUELEKEA UCHUMI WA VIWANDA

1278
0
Na Ismail Ngayonga
MAELEZO
DAR ES SALAAM
TANZANIA kama zilivyo nchi nyingine duniani inahitaji uchumi wa viwanda ili kuleta mageuzi ya haraka na kujenga msingi imara wa uchumi kwa kutumia ipasavyo rasilimali zilizopo na kukuza Pato la Taifa na kutoa nafasi nyingi na endelevu za ajira.
Uamuzi wa Serikali wa kujenga uchumi wa viwanda unalenga kuleta maendeleo jumuishi na endelevu ili kuiwezesha Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa kati inayoongozwa na viwanda ifikapo mwaka 2025 na kuwa chachu ya maendeleo ya sekta zinazohusiana na kuzalisha bidhaa bora kwa ajili ya masoko ya ndani na nje ya nchi.
Ujenzi wa uchumi wa viwanda unahitaji umadhubuti na nguvu za ziada katika kusimamia na kutekeleza kwa vitendo uvutiaji wa wawekezaji, ujenzi wa viwanda, kulea na kulinda viwanda vya ndani.
Sekta ya Viwanda Vidogo nchini ni sekta muhimu katika kutengeneza ajira, kukuza kipato na kuondoa umasikini, ambapo jumla ya jasiriamali milioni 3.1 zimeajiri asilimia 23.4 ya nguvu kazi ya Taifa na imechangia asilimia 27 katika Pato la Taifa.
Aidha, kulingana na takwimu za Sensa ya Viwanda ya mwaka 2013 iliyozinduliwa mwaka 2016, Tanzania ina jumla ya viwanda 49,243 ambapo asilimia 85.13 ni viwanda vidogo sana, asilimia 14.02 ni viwanda vidogo, asilimia 0.35 ni viwanda vya kati na asilimia 0.5 ni viwanda vikubwa.
Faida ya Sekta ya Viwanda Vidogo ni kuwa uanzishwaji wake hauhitaji elimu kubwa na mtaji mkubwa na hivyo vinaweza kuanzishwa katika eneo lolote la nchi, na hivyo mwanya mkubwa kwa vijana na wanawake kuanzisha viwanda na kujiajiri ambapo wasingepata fursa katika sekta nyingine zinazotoa ajira.
Akiwasiisha Hotuba ya Makadirio ya Bajeti ya Mapato na Matumizi kwa mwaka 2018/19, Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage anasema Serikali kupitia Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO) inaendelea na kutoa huduma za uendelezaji na uenezaji wa teknolojia kwa wajasiriamali wadogo nchini.
Anasema kuwa , SIDO inamiliki Vituo vya Maendeleo ya Teknolojia saba katika mikoa ya Arusha, Kigoma, Kilimanjaro, Iringa, Mbeya, Lindi na Shinyanga vinavyojihusisha na uendelezaji wa teknolojia na utengenezaji wa mashine na vipuli na kutoa huduma za kiufundi kwa wajasiriamali wadogo mijini na vijijini.
“Katika mwaka 2016/2017, jumla ya teknolojia mpya 30 zimetengenezwa na kuboreshwa kupitia vituo vya SIDO vya uendelezaji teknolojia (Technology Development Centre-TDCs) na huduma za ushauri wa kiufundi zilitolewa kwa wajasiriamali 3,433” anasema Mwijage.
Aidha Mwijage anasema katika mwaka 2016/17, Serikali iliendelea na Juhudi za kutafuta teknolojia kwa ajili ya mahitaji ya wajasiriamali wadogo, na jumla ya teknolojia73 zilipatikana kwa ajili ya matumizi ya wajasiriamali wadogo zikilenga uongezaji wa thamani ya mazao ya kilimo, upunguzaji wa matumizi ya miti na mazao yake, uchujaji wa asali na utengenezaji wa mishumaa.
Waziri Mwijage anasema katika kuimarisha mpango wa utoaji wa huduma za kiufundi kwa wajasiriamali wadogo vijijini, SIDO kupitia Mkakati wa Wilaya Moja Bidhaa Moja, katika mwaka 2016/2017jumla ya viwanda vidogo vipya 161 vilianzishwa na kutengeneza ajira 1,098 katika wilaya mbalimbali nchini.
Kwa mujibu wa Waziri Mwijage, SIDO imeendelea kutoa mafunzo mbalimbali ikihusisha  menejimenti, masoko, ubora, wa bidhaa, mbinu za uzalishaji mali, na uongozi wa vikundi/vyama kwa wajasiriamali ikiwa ni moja ya chachu ya kuimarisha na kuendeleza shughuli za biashara na miradi ya uzalishaji.
“Jumla ya wajasiriamali 5,750 kupitia kozi 230 wamepata mafunzo yaliyowawezesha kupata maarifa na stadi za kuimarisha shughuli zao za uzalishaji mali na mafunzo hayo yalifanyika mikoa yote nchini” anasema Mwijage.
Kuhusu huduma za masoko, Waziri Mwijage anasema Serikali kupitia SIDO imewezesha wajasiriamali kutambua hali na mahitaji ya soko kutokana na tafiti zilizofanyika na hushirikishwa katika maonesho mbalimbali ya bidhaa na huduma zinazoandaliwa na SIDO au Taasisi nyingine za ndani na nje ya nchi.
Anaongeza kuwa kupitia utaratibu huo, jumla ya maonesho matatu ya kanda yaliyowashirikisha wajasiriamali 603 yaliandaliwa na SIDO na kuwawezesha washiriki kufanya mauzo taslimu na oda ya Tsh. Milioni 237.7, ambapo imesaidia wajasiriamali licha ya kupata taarifa mbali mbali za biashara pia zimewezesha kutangaza bidhaa zao kupitia tovuti ya SIDO.
Akifafanua zaidi Waziri Mwijage anasema kupitia mifuko ya huduma za kifedha ikiwemo Mfuko wa Taifa wa Kuendeleza Wafanyabiashara na Wananchi (NEDF), na Mfuko wa Dhamana kwa Wajasiriamali Wadogo, Serikali kupitia SIDO imeweza  kutoa mikopo yenye thamani ya Tsh. Bilioni 3.92 kwa wajasiriamali 2,593 iliyowezesha kutoa ajira kwa watu 9,424.
Sekta ya Viwanda Vidogo ni msingi muhimu wa kuwandaa Watanzania kuwa wamiliki wa viwanda vya kati na viwanda vikubwa hapo baadaye, kwa kuwa hatua hiyo inawezesha kusambaa kwa viwanda nchi nzima pamoja na kupunguza wimbi la wananchi kutoka vijijini kuhamia mijini.

Leave a comment