Home Michezo SIMBA YATOA TAMKO KUHUSU RUFAA YAO FIFA NA KUHUSU PONGEZI ZA FIFA...

SIMBA YATOA TAMKO KUHUSU RUFAA YAO FIFA NA KUHUSU PONGEZI ZA FIFA KWA YANGA

178
0

Wakati ukiwa umesalia muda mfupi kabla ya kucheza mechi ya mwisho ya msimu huu wa 2016,2017 hapo kesho Jumamosi, Klabu ya Simba imetoa tamko kuhusu rufaa yao waliyoipeleka kwenye Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) wakidai pointi tatu.

Akizungumzia suala hilo, Makamu wa Rais wa Simba, Geoffrey Nyange maarufu kwa jina la Kaburu amesema kuwa suala lao bado lipo Fifa na taarifa kuwa shirikisho hilo limetuma salamu za pongezi za ubingwa wa Yanga ni jambo la kawaida ambalo limekuwa likifanywa na Fifa.

“Suala la Fifa kuitumia pongezi Yanga mbona ni jambo la kawaida ambalo Fifa imekuwa ikifanya kwa nchi zote ambazo zinafanikiwa kuwa bingwa, lakini hilo wala haliwezi kupindisha ukweli kuwa rufaa yetu haiwezi kufanyiwa kazi.

“Rufaa yetu bado ipo kwao na wanaifanyia kazi, ikitokea kukawa na mabadiliko, pointi tatu zikarejea kwetu kisha tukawa mabingwa, Fifa watatupa pongezi hata sisi kwa kuwa huo ni utaratibu wao,” alisema Kaburu.

Kuhusu kutojitokeza kwenye utoaji wa Tuzo za Ligi Kuu ya Vodacom zilizofanyika juzi Jumatano, Kaburu alisema wao wapo Dodoma na akili yao inawaza fainali ya Kombe la FA ambapo timu yao inatarajiwa kucheza dhidi ya Mbao FC kwenye Uwanja wa Jamhuri mkoani Dodoma.

Kaburu amesema kama ni suala la zawadi za tuzo hizo wao watazikuta na watazichukua lakini kuhusu kususia tuzo hizo hakutaka kulizungumzia suala hilo kiundani.

Ikumbukwe kuwa Simba imekata rufaa kupinga TFF kuipa Kagera Sugar kumtumia beki Mohamed Fakhi wakidai alikuwa na kadi tatu za njano jambo ambalo liliwafanya wao wakate rufaa na kupewa pointi katika mchezo huo ambao Simba ilifungwa mabao 2-1, baada ya maamuzi hayo baadaye yalibadilika na TFF kutangaza kurejesha matokeo kama yalivyokuwa awali kutokana na upungufu uliojitokeza wakati Simba ikikata rufaa.