Home News SportPesa YAMTAMBULISHA BONDIA HASSAN MWAKINYO KUWA BALOZI WAKE

SportPesa YAMTAMBULISHA BONDIA HASSAN MWAKINYO KUWA BALOZI WAKE

1071
0
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
KAMPUNI ya kubashiri michezo ya Sportpesa Tanzania imemtambulisha bondia Hassan Mwakinyo kama balozi wa kampuni hiyo.
Bondia huyo ambaye kwa sasa ndio anayeongoza katika Ukanda huu wa Afrika Mashariki na Kati katika Uzani wa Super Welter ameingia katika makubaliano ya miaka mitatu huku akiwakilisha kampuni hiyo kwenye matukio yake muhimu.
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam wakati wa kumtambulisha bondia hiyo, Mkurugenzi wa Utawala na Utekelezaji Sportpesa Tanzania Tarimba Abbas alisema kuwa kampuni ya Sportpesa kudhamini michezo imekuwa ni jambo la kawaida.
“Kampuni yetu mama ya Sportpesa Kenya ambayo ilianzishwa 2014 imekuwa ikidhamini michezo mingi kama mpira wa miguu, rugby, mchezo wa ngumi na ligi kubwa duniani,” alisema Tarimba.
“Na kwa sababu hiyo, Sportpesa Tanzania kwa sasa inafuata njia hiyo kwa kudhamini michezo ya ngumi nchini. Tulianza na mpira wa miguu na sasa tumeingia kwenye mchezo wa ngumi kwa bondia Hassan Mwakinyo kuwa balozi wa Sportpesa kwa mkataba wa miaka mitatu,” aliongeza.
Alisema wanaamini kwamba kumdhamini bondia huyo kuteleta changamoto mpya na kuwa chachu ya kuibua mabondia wengine na kuongeza ushindani na kujiamini hususani kwenye mapambano ya kimataifa.
Aidha alisema kuwa wakati kampuni hiyo ikiendelea katika hatua mbalimbali za ukuaji, wanataka pia kukua na Mwakinyo na kuleta mwanga mpya kwenye mchezo huu wa ngumi nchini.
Bondia huyo mwenye umri wa miaka 23 na mwenye rekodi ya (13-2,8 KOs) alisema anajisikia furaha sana kwa kampuni ya Sportpesa kutambua kipaji chake na kuweza kumuunga mkono kwa kumpa udhamini wa miaka mitatu ambao ni wa kwanza na wa pekee na hasa kwenye upande wa mchezo wa ngumi nchini.
“Hii ni muhimu kwangu kwani itaniongezea hamasa na kunifanya nizidi kujulikana zaidi, imeniongezea kujiamini na nataka niwaahidi ya kwamba nitazidi kuongeza bidii ili nizidi kupata mafanikio mimi binafsi lakini pia kwa nchi yangu ya Tanzania,” alisema Mwakingyo.
Alisema kuwa kuchaguliwa kuwa balozi wa kampuni hiyo ni ishara nzuri kwake na kwa sekta ya mchezo wa ngumi nchini.
“Nachukua fursha hii kutoa pongezi kwa serikali, kwa kufanya kzi kwa bidii na hatimaye kuweza kurudisha nidhamu ya mchezo wa ngumi nchini na hatimaye tumeanza kufaidika kwa kupata wadhamini kama Sportpesa,” aliongeza.
Kwa upande wake Wzairi wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dk. Harrison Mwakyembe aliwapongeza kampuni ya Sportpesa kwa kumchagua Hassan Mwakinyo kuwa balozi wake.
“Kwa udhamini huu, inaonyesha ni jinsi gani Sportpesa wamejitolea kukuza michezo hapa nchini. Vile vile inaonyesha imani yetu kwenye mchezo wa ngumi, hii ni hatua njema na naomba makampuni mengine kuiga mfano wa Sportpesa,” alisema Dk. Mwakyembe.
Waziri Mwakyembe alimpongeza Mwakinyo huku akisema ni mmoja wa mabondia wazuri ambao Tanzania ishawahi kuwa nao. Hata hivyo alimtaka kuheshimu mkataba wa udhamini wake kwani kutamjengea heshima na kupata wadhamini wengine zaidi.
Septemba mwaka huu, Hassan Mwakinyo alifanya mambo makubwa baada ya kumchapa Muingereza Sam Eggington kwa Technical Knock Out kwenye raundi ya pili katika pambano lililokuwa na raundi 10 la uzani wa Super Welter ambalo lilifanyika kwenye ukumbi wa Barclayeard kule Birmingham, Uingereza. Ushindi huo ulimfanya kufikisha pointi 115 na kushika nafasi ya 16 duniani na nafasi ya kwanza Afrika kwa uzani wa Super Welter.