Home News Tanzania mwenyeji zoezi la ushirikiano wa Majeshi EAC

Tanzania mwenyeji zoezi la ushirikiano wa Majeshi EAC

1215
0

Na Abraham Ntambara, Dar es Salaam

TANZANIA inatarajiwa kuwa mwenyeji wa zoezi liitwalo USHIRIKIANO IMARA 2018 ambapo Majeshi ya Ulinzi na Usalama kutoka nchi zote za wanachama wa Afrika Mashariki yatashiriki.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam Mkuu wa Tawila Mafunzo na Utendaji Kivita Jeshini Meja Jenerali Alfredi Kampinga alisema zoezi hilo ni la Medani (FTX) litafanyika katika mkoa wa Tanga Wilaya ya Tanga Mjini na Wilaya ya Muheza kuanzia Novemba 5, 2018 hadi Novemba 21, 2018.

“Kama mtakumbuka Baada ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kuundwa upya mwaka 2001 nchi wanachama zilitiliana saini mkataba wa makubaliano ya ushirikiano katika masuala ya kiulinzi ( MoU on Coorperation in Defence Affairs) ambapo eneo mojawapo ikiwa ni mazoezi ya pamoja ya kijeshi,” alisema Meje Jenerali Kapinga.

Alisema wanategemea wanajeshi, polisi na washiriki wengine kutoka Taasisi za serikali wanaokadiriwa kufikia idadi ya 1250 kutoka nchi ya Burundi, Kenya, Rwanda, Uganda na Tanzania kushiriki zoezi hilo. Kutokana na nchi ya Sudani Kusini kusaini Mikataba ya Amani wametoa udhuru wa kutoshiriki zoezi hilo.

Meja Jenerali Kapinga alisema dhumuni la zoezi hilo ni kuyajengea uwezo Majeshi yetu katika kukabiliana na changamoto mbalimbali za kiulinzi na kiusalama ambazo ni ugaidi, uharamia na kutoa msaada wakati wa majanga.

Aidha aliongeza kuwa zoezi hilo pia limeandaliwa ili kuyafanya majeshi yetu kuwa na weledi katika utendaji wao wa majukumu wakati wa operesheniza ulinzi wa Amani.

Alisema dhumuni lingine ni kubadilishana uzoefu wa kiutendaji, kuimarisha mahusiano baina ya nchi zetu, Majeshi yetu ya Afrika Mashariki pamoja na Taasisi zingine za kiraia ambazo zitashiriki zoezi hili.

Alieleza kwamba katika zoezi hilo kutakuwa na kazi za kusaidia jamii kama vile ujenzi wa madarasa, ujenzi wa ofisi za walimu pamoja na vyoo katika shule ya msingi ya Machemba iliyopo wilaya ya Muheza Mkoani Tanga.

Pia kutakuwa na utoaji wa Huduma za tiba kwa wananchi katia eneo la zoezi.

Alitoa wito kwa wananchi wa Tanga kuendeleo kutoa ushirikiano kwa kipindi chote watakachokuwa huko.