Home News TCU YAZUIA VYUO VIKUU VINNE KUFANYA UDAHILI, YAAMURU WANAFUNZI WANAOENDELEA NA MASOMO...

TCU YAZUIA VYUO VIKUU VINNE KUFANYA UDAHILI, YAAMURU WANAFUNZI WANAOENDELEA NA MASOMO WAHAMISHWE

1513
0

Katibu Mtendaji wa Tume ya Vyuo Vikuu nchini (TCU) Prof. Charles Kihampa akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) jijini Dar es Salaam.

Na Abraham Ntambara, Dar es Salaam

TUME ya Vyuo Vikuu Nchini (TCU) imezuia Vyuo Vikuu vinne kufanya udahili wa wanafunzi wapya na kuamuru kuhamishwa wengine  wa shahada ya kwanza wanaoendelea na masomo kwa mwaka 2018/2019.

 

Hayo yalibainishwa leo jijini Dar es Salaam na Katibu Mtendaji wa TCU Profesa Charles Kihampa, alipokuwa akiongea na waanshi wa habari, alitaja vyuo hivyo kuwa ni Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Tiba na Teknolojia (IMTU)-Dar es Salaam na Chuo Kikuu Kishiriki cha Askofu Mkuu James (AJUCo), Songea-Ruvuma.

Vingine ni Chuo Kikuu Kishiriki cha Kumbukumbu ya Stefano Moshi (SMMUCo), Moshi-Kilimanjaro na Chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Sebastian Kolowa (SEKOMU), Lushoto-Tanga.

“Tume imezuia udahili wa wanafunzi wapya na kuamuru kuhamishwa mara moja wanafumzi wa shahada ya kwanza wanaoendelea na masomo kwa mwaka 2018/2019 katika jumla ya programu tisa (9) za shahada ya kwanza kutoka Vyuo Vikuu vinne,” alisema Prof. Kihampa.

Katika hatu nyingie TCU imekifutia usajili wa kituo cha Chuo Kikuu Kishiriki cha Kumbukumbu ya Stefano Moshi (SMMUCo) na kuamuru wanafunzi wote wanaoendelea na masomo wahamishwe.

“Tume imefuta usajili wa kituo cha mjini Moshi cha Chuo Kikuu Kishiriki cha SMMUCo-Town Centre na kuamuru wanafunzi wote wanaoendelea na masomo ahamishiwe katika kampasi kuu ya chuo hicho iliyopo Masoka, Moshi-Kilimanjaro,” alieleza Prof. Kihampa.

Alibainisha kuwa wameendela kusitisha udahili wa wanafunzi wapya kwa ngazi zote za masomo katika vyuo vikuu viwili ambavyo ni Chuo Kikuu Kishiriki cha Afya na Sayansi Shirikishi cha Mt. Fransisko (SFUCHAS), Ifakara-Morogoro na Chuo Kikuu Kishiriki cha Askofu Mkuu Mihayo Tabora (AMUCTA), Tabora.

Aidha alisema, wamelidhia ombi la Chuo Kikuu Kishiriki cha Kumbukumbu ya Stefano Moshi (SMMUCo), Moshi-Kilimanjaro kuhamisha wanafunzi wa programu za Certificate in Hospitality and Tourism Studies, Diploma in Mass Communication na Certificate ni Mass Communication.

Mapendekezo Mahsusi

Alitaja mapendekezo hayo kuwa ni pamoja na kuvitaka vyuo vikuu vyote vilivyotajwa kuzingatia na kutekelea maelekezo yao mara moja, Vyuo Vikuu vyote vinavyotakiwa kuhamisha wanafunzi vimeagizwa kufuata taratibu za uhamisho na kukamilisha zoezi la uhamisho wa wanafunzi ndani ya wiki mbili kuanzia Novemba 7, 2018.

Katibu Mtendaji huyo alibainisha maependekezo mengine ni kwamba vyuo vikuu vyote ambavyo wanafunzi wao wanatakiwa kuhama vimeagizwa kuasiliana haraka na vyuo wanavyotakiwa kuhamia na kuwasilisha taarifa zote za wanafunzi kwa vyuo wanavyohamia.

Na mwisho vyuo vyote vilivyoelekezwa kuhamisha wanafunzi, vimeagizwa kuwaarifu mara moja wanafunzi wote kuhusu vyuo wanavyotakiwa kuhamia kama walivyoelezwa.