Home News ULIMWENGU AWATAKA WANANCHI, VIONGOZI NCHINI KUTENDA HAKI KWA WENGINE

ULIMWENGU AWATAKA WANANCHI, VIONGOZI NCHINI KUTENDA HAKI KWA WENGINE

940
0

Mwandishi Nguli nchini Jenerali Ulimwengu, akizungumaza kwenye kongamano la Haki na Wajibu wa Raia lililoandaliwa na jukwaa la Change Tanzania jijini Dar es Salaam.

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

WANANCHI na Viongozi nchini wametakiwa kutenda haki kama watakavyo watu wengine wawatendee wao.

Hayo yalisemwa jana jijini Dar es Salaam na Mwandishi Mkongwe nchini Jenerali Ulimwengu, katika kongamano kuhusu haki na wajibu wa raia lililoandaliwa na Jukwaa la Change Tanzania.

“Tunatakiwa kutenda haki kwa kila mtu na kuachana na tabia kama za viongozi kufanya mambo ya uvunjifu wa haki kwa kutumia kigezo cha kutekeleza maagizo kutoka juu bila kujali athari zake,” alisema Ulimwengu.

Mkurugenzi Mtendaji wa Jukwaa la Change Tanzani Maria Sarungi, akizungumaza kwenye kongamano la Haki na Wajibu wa Raia lililoandaliwa na Jukwaa hilo jijini Dar es Salaam.

Adha aliwausia viongozi na vijana walioshiriki katika jukwaa hilo kutetea watu wasiowajua, wanyonge, kuwa waaminifu zaidi ya kuwa watiifu, kushiriki katika maendeleo ya nchi, kukemea maovu na kutenda mema.

Pamoja na hayo Mwandishi huyo nguli amewataka wanaharakati kutokuogopa kufa kwa sababu ya kutetea haki kwani kuogopa hilo ni ujinga.

“Kila mtu atakufa bila kujali sababu, kufa ni suala la muda tu na kuogopa kufa ni ujinga, bora kufa kwa kutetea jambo la maana kuliko kufa kwa mambo ya upuuzi, alisema Ulimwengu.

Pichani ni baadhi ya wananchi waliohudhuria kwenye kongamano.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Jukwa hilo, Maria Sarungi alisema jukwaa hilo ambalo lilianzishwa mwaka 2012, malengo yake ni kuelimisha na na kusaidia wanachama wake watakaoathirika na sheria ya makosa ya mitandaoni.

Aliongeza mengine ni kukumbusha wanachama wajibu wao wa msingi na kuimarisha mtandao wa uanaharakati katika mabadiliko chanya na kuunganisha vijana kutafakari na kujenga maarifa juu ya haki na wajibu wao kwa Taifa katika maamuzi badala ya kuwaachia wanasiasa.

Naye Mratibu wa Taifa wa Change Tanzania Mshabaha Mashabaha alisema hilo ni jukwa la pili kuanzishwa na asasi hiyo tangu 2016.

“Change Tanzania ni harakati zinazosukuma na kuhamasisha maendeleo kwa kutumia mitandao ya kijamii, kusimamia uhuru wa kujieleza wa wananchi ikiwa ni pamoja na kutoa fursa kwa wananchi kujadili, kukosoa na kutoa taarifa kupitia mitandao,” alifafanua Mshabaha.

Hata hivyo mwakilishi kutoka Taasisi ya Twaweza Annastazia Rugaba akichangia katika jukwaa hilo alisema matamanio yake ni kuona vijana wakijengewa uwezo na fikra mpya za kutambua wajibu wao kwa Taifa badala ya kuwa walalamikaji tu mitandaoni wakidai haki zao au kukosoa uwajibikaji wa viongozi.