Home News WALIOVAMIA MSITU WA NAMWAI WAPEWA SIKU 14

WALIOVAMIA MSITU WA NAMWAI WAPEWA SIKU 14

1209
0
Na. Andrew Chimesela – Morogoro
Wananchi waliovamia msitu wa Namwai  ambao upo Wilaya ya Kilombero Mkoani Morogoro, wamepewa siku 14 za kutojihusisha na shughuli za kibinadamu katika msitu huo, kuboboa makazi yao na kuondoka, vinginevyo wataondolewa kwa nguvu kwa mujibu wa sheria ya misitu ya mwaka 2002.
Agizo hilo limetolewa Novemba Mosi mwaka huu na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Kebwe Stephen Kebwe wakati wa ziara yake Wilayani Kilombero ambapo pamoja na mambo mengine alitembelea msitu huo na kuona uharibifu mkubwa uliofanyika, na kulaimika kutoa agizo hilo wakati wa mkutano wake na wananchi wa Kijiji cha Ihenga.
Dkt. Kebwe amesema, ameamua kutoa tamko hilo baada ya kujiridhisha kuwepo kwa uharibifu mkubwa wa msitu huo kwani ni msitu pekee wa mapito ya wanyama (corridor) kutoka milima ya Udzungwa  na Hifadhi ya Msitu wa Mazingira Asilia wa Kilombero kuelekea pori la Akiba la Selous.
Kwa sababu hiyo, Dkt. Kebwe ametoa siku 14 kuanzia Novemba Mosi mwaka huu, watu wote wanaofanya shughuli za kibindamu ndani ya msitu wa Namwai kuondoka, na atakayekaidi  agizo hilo ataondolewa kwa nguvu na kulipa gharama za kumuondoa. “leo tarehe moja siku kumi na nne, MWISHO TAREHE KUMI NA NNE” alisisitiza Dkt. Kebwe.
Sambamba na agizo hilo Dkt. Kebwe amewaagiza wataalamu  wa Ardhi na Misitu kutoka Ofisi ya Wilaya ya Kilombero wakishirikiana na Wataalamu kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro kufanya utambuzi wa mipaka ya msitu huo na kuweka alama kuzunguka msitu wote ili kutambua mipaka halisi ya msitu huo huku akiwatahadhalisha wale watakaodiriki kuharibu alama hizo kuchukuliwa adhabu kali za kisheria.
Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa Mkoa amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Kilombero James Ihunyo kuwachukulia hatua kali za kinidhamu Viongozi wa Kijiji cha Kisegese walioshiriki katika kugawa maeneo ya mashamba ndani ya Msitu huo.
Wakati huo huo Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero Mhe. Daud ligazio amesema, kwa muda mrefu walikuwa wanatafuta njia ya kuwaondoa wavamizi wa msitu wa Namwai bila mafanikio na kwamba sasa anaamini kwa agizo la Mkuu wa Mkoa msitu huo utabaki salama, huku Diwani wa Kata ya Mofu ambapo msitu huo upo Bw. Redfred Magungu akipongeza maagizo ya Mkuu wa Mkoa.
Naye Danford Mateso ambaye alimuwakilishi Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Clifford Tandari katika ziara hiyo ya Mkuu wa Mkoa, aliwataka wananchi waliovamia msitu wa Namwai kuondoka kwa hiari yao kabla Mkono wa sheria haujawafikia.
Awali akitoa taarifa kwa Mkuu wa Mkoa, Afisa Ardhi na  Maliasili Wilaya ya Kilombero Bw. Joseph Mgana ametaja changamoto wanazokutana nazo katika jitihada za kuunusuru Msitu wa Namwai kuwa ni pamoja na kutopewa ushirikiano wa kutosha kwa baadhi ya Mamlaka ikiwemo Mahakama  ambapo baadhi ya watuhumiwa waliofikishwa mahakamani takribani mara mbili kwa tuhuma za kuvamia msitu huo waliachiwa mara zote katika mazingira ya kutatanisha.
Huku Afisa Misitu Bw. Magai Falence amesema wananchi ambao wako ndani ya msitu wa Namwai wamevunja sheria ya misitu ya mwaka 2002 kipengele cha 26 (“a – s”) ambacho kinazuia shughuli za kibinadamu kufanyika ndani ya misitu ya Hifadhi.
Nao wananchi wa Kijiji cha Ihenga Kijiji kilichotokana na Kijiji mama cha Mofu Bw. Edward Paulo na Magdalena Silvester nao wamepongeza agizo la Mkuu wa Mkoa kwa kile walichoeleza kuwa walikuwa wananufaika kwa namna mbalimbali na msitu huo kabla haujavamiwa.
Msitu wa Namwai ambao una zaidi ya hekta 1,833 ulitengwa kwa mujibu wa Sera ya Misitu ya mwaka 1998 na sheria ya misitu namba 14 ya mwaka 2002 kuwa Hifadhi ya Kijiji cha Mofu tangu mwaka 2004 ambacho ni kijiji mama ya Kijiji cha Ihenga kinachomiliki msitu huo kwa sasa.
Taarifa iliyosomwa mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro imeeleza kuwa kuna Matamko kadhaa yaliyokwisha tamkwa kutaka wavamizi kuondoka katika Msitu wa namwai bila mafanikio. Matamko hayo ni pamoja na tamko la Serikali ya Kijiji mama cha Mofu lililotolewa mwaka 2011 kuwataka watu wote wanaofanya shughuli za kibinadamu ndani ya msitu huo kuondoka lakini agizo hilo halikutekelezwa.
Aidha, aliyewahi kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kilombero Hassan Masala aliwahi kutoa matamko kwa vipindi viwili tofauti Aprili 2014 na Februari 2017 ya kuwataka wavamizi katika msitu huo wa Namwai kuondoka lakini maagizo hayo yote yalipuuzwa.