Home News WAZIRI MKUU KASSIM MAJALIWA MGENI RASMI MAADHIMISHO YA 73 YA UN

WAZIRI MKUU KASSIM MAJALIWA MGENI RASMI MAADHIMISHO YA 73 YA UN

1465
0
Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa, anatarajiwa Kesho kuwa mgeni rasmi katika maadhimisho ya kumbukumbu ya 73 tangu kuanzishwa kwa Umoja wa Mataifa (UN).
Kuanzishwa kwa UN kunasherehekewa kote ulimwenguni kila Oktoba 24 ya kila mwaka ambapo maadhimisho ya mwaka huu yatafanyika jijini Dar es Salaam yakibeba ujumbe: ‘Uwezeshaji Vijana na Ubunifu kwa ajili ya Malengo ya Maendeleo Endelevu.’
Katika maadhimisho hayo bendera ya UN itapandishwa huku tukio hilo likitarajiwa kuhudhuriwa na wajumbe wa jumuiya ya kimataifa, Wakuu wa Mashirika ya UN nchini Tanzania, Vijana, Vyama vya Kiraia, Vyombo vya habari na wadau wengine.
Akizungumzia maadhimisho hayo leo jijini Dar es Salaam Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk. Damas Ndumbaro (MB) aliangazia ushirika endelevu baina ya UN na Vijana kutafuta mbinu za kiubunifu ili kushiriki katika ufikiwaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) mwaka 2030.
“Tanzania ikiwa moja ya nchi wanachama wa umoja huo, imekuwa ikishirikiana na Mashirika ya Umoja wa Mataifa, Taasisi, Mifuko ya fedha iliyopo chini yake, na programu mbalimbali katika kuimarisha amani, maendeleo ya kijamii na kuboresha hali ya uchumi kwa wananchi wa maeneo mbalimbali nchini,” alisema Dk. Ndumbaro.
Dk. Ndumbaro aliongeza kwamba “Kaulimbiu ya miaka 73 ya Umoja wa Mataifa inaweka mkazo katika kuwezesha vijana wa Taifa letu kubuni shuguli mbalimbali zitakazowaingizia kipato cha kila siku. Serikali na Umoja wa Mataifa tumeona umuhimu wa kuendelea kuwajengea uwezo vijana wetu ambao ni nguvu kazi ya Taifa,”.
Kwa upande wake, Mratibu Mkazi wa UN nchini, Alvaro Rodriguez, alipongeza utayari wa vijana wa kutekeleza ahadi ya kuingia kwenye uchumi wa viwanda na nchi kufika hadhi ya kipato cha kati ifikapo mwaka 2025 huku akieleza kwamba vijana ni muhimu sana katika kufikiwa kwa lengo hilo.
“Vijana¬† hawana budi kupokea kijiti katika kuyamiliki malengo SDGs. Malengo haya ya SDGs si wajibu wa UN au serikali bali yanahitaji ushiriki wa kila mmoja,” alisema Rodriguez.
Aliongeza “Malengo ya SDGs yanatoa wito kwamba asiachwe yeyote nyuma na tunapoazimisha Siku ya UN, hebu turudie ahadi yetu kwa kuhakikisha kwamba vijana wote nchini wanapata fursa ya kushiriki katika utekelezaji wa FYDP II na SDGs,”
Kupitia ushirikiano kati ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Ofisi ya Waziri Mkuu na Umoja wa Mataifa Tanzania kwa kushirikiana na washirika wengine maadhisho ya mwaka huu yatalenga vijana kwa mujibu wa ujumbe. “Uwezeshaji Vijana na Ubunifu ili kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs).
Serikali na UN kwa pamoja zinahimiza ushiriki kamilifu wa vijana katika utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Pili wa Miaka Mitano wa Maendeleo (FYDP II) na Maendeleo Endelevu (SDGs).