Home News WAZIRI MPINA ATOA SIKU SABA KWA MAKATIBU WAKUU WA KILIMO NA MIFUGO

WAZIRI MPINA ATOA SIKU SABA KWA MAKATIBU WAKUU WA KILIMO NA MIFUGO

100
0
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina akizungumza.
Na John Mapepele
Waziri
wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina ametoa siku saba kwa makatibu wakuu wa
Kilimo na Mifugo kuwasilisha wizarani kwake taarifa ya kwanini bei ya
mbegu za mahindi na mtama pamoja na gharama za uhimilishaji mifugo
nchini ni kubwa licha ya uwepo wa usimamizi wa Serikali,pia kuendelea
kuagiza mbegu za matunda na mbogamboga nje ya nchi ambazo zinaweza
kuzalishwa hapa nchini.
Mbali na hilo, Waziri Mpina pia
amezitaka Taasisi za TPRI,TFDA,TBS na Kurugenzi ya Huduma za Mifugo
katika Wizara ya Mifugo na Uvuvi kujitathmini upya utendaji kazi wao
kama wanastahili kuwepo baada ya kushamiri kwa dawa na viuatilifu vya
kilimo na mifugo feki na vilivyokwisha muda wa matumizi na kusababisha
hasara kubwa kwa wakulima,wafugaji na Taifa kwa ujumla.
Akifungua
maonesho ya Kilimo Nane Nane, Kanda ya Kaskazini yanayofanyika katika
viwanja vya Themi jijini Arusha, Waziri Mpina alisema ni jambo la aibu
kwa viongozi kuendelea kuwakutanisha wakulima na wafugaji katika
maonesho hayo kila mwaka huku changamoto zao za msingi ikiwemo kuuziwa
mbegu kwa bei kubwa, dawa na viuatilifu visizoua wadudu kwenye mazao na
mifugo yao zikiwa hazijapatiwa ufumbuzi.
Alisema baadhi ya
wazalishaji wa mbegu za kilimo nchini wamekuwa wakiuza kwa bei kubwa
kiasi cha kuwakatisha tamaa wakulima kutumia mbegu bora ambapo baadhi ya
kampuni zimekuwa zikiuza kilo moja ya mbegu ya mahindi kwa sh. 6,000
wakati bei wanayonunua kwa wakulima wa kilimo cha mkataba cha uzalishaji
mbegu kwa kilo ni sh 1,200 na bei ya mahindi ya kawaida kwa kilo ni
sh. 600 tu.
Pia gharama za uhamilishaji mifugo nchini dozi moja
huuzwa wastani wa sh 3,000 kutoka katika vituo vya Taifa vya
uhamilishaji mifugo lakini kampuni binafsi za uhamilishaji huwatoza
wafugaji wastani wa sh 20,000 hadi sh 40,000 kwa dozi, gharama ambazo
wafugaji wengi hawawezi kuzimudu.
Pia Waziri Mpina aliagiza
Halmashauri zote nchini kuhakikisha zinakuwa na shamba darasa la bwawa
la ufugaji wa samaki ili kuongeza upatikanaji wa chakula na biashara ya
mazao ya uvuvi, ajira na mapato ya Serikali.
Kuhusu sekta ya
mifugo Waziri Mpina alisema licha ya mikoa hiyo ya Kilimanjaro, Arusha
na Manyara kuwa na takribani asilimia 15 ya mifugo yote nchini lakini
hakuna kiwanda hata kimoja cha kuchakata mazao ya mifugo hali ambayo
inasababisha mifugo mingi kutoroshwa nchi jirani ya Kenya ajili ya
kutafuta masoko.
Pia aliagiza halmashauri zote nchini kufanyia
matengenezo na ukarabati minada,machinjio na majosho ili kuongeza tija
katika uzalishaji na ukusanyaji maduhuli yatokanayo na sekta ya mifugo
Kuhusu
maendeleo ya sekta ya uvuvi, Waziri Mpina alisema kanda ya kaskazini
inayo fursa kubwa ya uvuvi katika Ziwa Eyasi, Duluti, Manyara,
Babati,Buruge, Bassotu, Jipe, Chala na Karamba na katika Bwawa la Nyumba
ya Mungu, Kalemawe na mabwawa ya kuchimba ambapo aliagiza kufanyika kwa
uvuvi endelevu na kuachana na uvuvi haramu.
Serikali pia
inakusudia kukiboresha zaidi kituo cha kuzalisha vifaranga vya samaki
Tanga ili kiweze kuchochea ufugaji samaki kwenye mabwawa katika kanda
hiyo.
Alisema ni jambo la aibu Taifa kuendelea kutumia mabilioni
ya fedha kuagiza samaki kutoka nje ya nchi wakati fursa kubwa za
uwekezaji kwenye sekta hiyo zipo hapa nchini na kwamba Serikali ya
awamu ya tano imejipanga kuhakikisha uzalishaji wa samaki nchini
unaongezeka.
Kwa upande wake Katibu Tawala Mkoa wa Arusha,
Richard Kwitega alisema kanda ya kaskazini ina jumla ya ng’ombe milioni
4.4, Mbuzi milioni 4.1, Kondoo milioni 2.7 na kwamba bado haijaweza
kunufaisha vya kutosha kanda hiyo na kuahidi kusimamia kikamilifu
maagizo mapya ya Waziri Mpina ili kuhakikisha sekta za Kilimo na Mifugo
zinatoa mchango unaostahili kwa maendeleo ya kanda hiyo na Taifa kwa
ujumla.