YANGA YAIPEPERUSHA VYEMA BENDERA YA TANZANIA UGENINI - The Choice

YANGA YAIPEPERUSHA VYEMA BENDERA YA TANZANIA UGENINI

0

Mabingwa Watetezi wa Comoro timu ya Ngaya FC imeanza vibaya katika Michuano ya awali ya Kombe la Ligi ya Mabingwa barani Afrika baada ya kukubali kichapo cha Paka Mwizi toka kwa Mabingwa wa kihistoria nchini Tanzania Yanga cha jumla ya Magoli 5-1 na kujiweka katika nafasi finyu ya kusonga mbele.

Aidha, dakika ya 43 kiungo mkabaji toka Zambia, Justine Zullu alifunga bao la kwanza baada ya kupokea pasi toka kwa Obrey Chirwa na Simon Msuva alifunga la pili dakika ya 45 kwa shuti la Mita 18 ambalo lilimshinda Mlinda Mlango wa Ngaya Said, hadi mapumziko Yanga walikuwa mbele kwa magoli mawili.

Kipindi cha pili kilianza kwa timu zote kufanya mabadiliko hata hivyo wanajangwani waliweza kutumia nafasi ambazo waliweza kuzipata Obrey Chirwa alifunga la tatu dakika ya 59 baada ya Kamusoko kupigia pande la pasi na dakika ya 65 Mshambuliaji mwenye rekodi ya Tuzo Tanzania Amis Tambwe alifunga la nne akipokea krosi toka kwa beki Juma Abdul.

Akitokea benchi Said Khalfan aliifungia Ngaya bao la kufutia machozi baada ya kuwazidi ujanja mabeki wa Yanga dakika ya 66 hata hivyo furaha yao haikuweza kudumu kwani dakika ya 73 Juma Mahadhi alipigilia msumari wa tano kwa pasi safi toka kwa Thabani Kamusoko.

Hadi mwamuzi anamaliza Mpira Yanga wameibuka na ushindi wa jumla ya magoli 5-1 na kujiweka katika nafasi nzuri ya kusonga mbele hatua inayofuata na timu hizo zinatarajia kurudiana Februari 18 jijini Dar es salaam.

Facebook Comments
Share.

About Author