Boban, Nyosso wahusishwa Simba - The Choice

Boban, Nyosso wahusishwa Simba

0

Nyosso

KLABU ya Simba imechemsha kwa mara nyingine katika Ligi Kuu Bara msimu huu, ikiukosa ubingwa na hata tiketi za mechi za kimataifa, lakini kumbe nyuma ya kuyumba huko kumehusishwa na wakongwe wake wa zamani.

Viungo Haruna Moshi ‘Boban’ na Ramadhani Chombo ‘Redondo’ na beki Juma Nyosso wamehusishwa kwa kuyumba kwa timu hiyo kwa misimu mfululizo, huku Katibu Mwenezi wa zamani, Said ‘Seydou’ Rubeya akifichua kuwa watani zao Yanga wana ukata kama wao ila wanatumia akili na hekima kumaliza matatizo.

Amri Kiemba aliyewahi kuichezea timu hiyo, alisema Simba haihitaji  kusaka mchawi, matatizo yao yamesababishwa na kutimua wakongwe wote klabuni na kuja na kauli mbiu ya kutengeneza timu chipukizi, imewagharimu.

Alisema hata hivyo mipango iliyokuwa ikitangazwa ilipuuzwa kwa nyota wote chipukizi kutimuliwa na kuifanya timu iyumbe.

“Simba, ilianza kupoteza mwelekeo wa ubingwa ilipotimua wakongwe kina Boban, Nyoso na wengine wakiwadanganya mashabiki wanajenga timu kabla ya kuwaachia chipukizi wakali kina Ramadhan Singano, William Lucian, Abdallah Seseme, Edward Christopher na wengine,” alisema.

Alisema timu inapomuondoa mchezaji fulani lazima kwanza iwe imepata mbadala kitu ambacho hakikufanyika Msimbazi. Naye Seydou alisema Simba imejaa majungu ndio maana inashindwa kuhimili vishindo kama Yanga aliodai hata wao ni njaa kali ila wajanja katika kuvumilia.

“Simba kumejaa majungu ndiyo maana inatimua ovyo wachezaji na makocha kwa kisingizio eti wameuza mechi, Yanga wajanja wana watu wanaochunguza kabla ya kuamua,’’ alisema.

Alisema wachezaji wote walitimuliwa Simba kwa mizengwe leo ndio wanaong’ara klabu nyingine ikiwamo Yanga, kama Amissi Tambwe, Kelvin Yondani, Deo Munishi ‘Dida’, Ally Mustapha ‘Barthez’, Elias Maguli na sasa Kessy (Hassan.).

Share.

About Author