Home News CDF: Vitendo vya ukatili kwa wanawake na watoto vinaongezeka

CDF: Vitendo vya ukatili kwa wanawake na watoto vinaongezeka

881
0

Na Abrahama Ntambara, Dar es Salaam

PAMOJA na Juhudi za Serikali na Wadau mbalimbali katika kutokomeza vitendo vya ukatili kwa wanawake na watoto nchini, Shirika la Jukwaa la Utu wa Mtoto (CDF) limesema vitendo hivyo vimekuwa vikiongezeka.

Hayo yameelezwa jana jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mtendaji wa CDF Koshuma Mtengeti alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari juu ya kongamano waliloandaa la kitaifa kujadili hali ya ukatili dhidi ya wanawake na watoto nchini na namna yakutokomeza vitendo hivyo.

Mtengeti alisema kwa mujibu wa Utafiti wa Demografia na Afya wa mwaka 2015/2016 unaonesha kuwa idadi ya wasichana wanaopata watoto katika umri wa miaka 15-19 imeongezeka mpaka kufikia asilimia 27 mwaka 2015, kutoka asilimia 23 mwaka 2010.

“Halikadhalika, Utafiti huo umeonyesha kuwa asilimia 40 ya wanawake wenye umri kati ya miaka 15-49 wamefanyiwa vitendo vya ukatili wa kimwili tangu wakiwa na umri wa miaka 15,” alisema Mtengeti.

“Asilimia 17 ya wanawake wenye umri kati ya miaka 15-49 wameshafanyiwa vitendo vya ukatili wa kingono katika kipindi cha miezi 12 iliyopita (wakati wa utafiti). Tafiti zimeendelea kubainisha kuwa asilimia 50 ya wanawake walioolewa walifanyiwa vitendo vya ukatili wa kimwili, kingono au kihisia,” aliongeza.

Aliitaka jamii kutambua kwamba vitendo vya ukatili dhidi ya watoto ni suala zito la haki za binadamu, jamii na afya ya jamii nchini Tanzania kama ilivyo katika nchi nyingine duniani. Vitendo hivi vinamomonyoa msingi imara ambao watoto wanahitaji ili wawe na afya bora na maisha yenye tija, na vinasigana na haki ya msingi ya wanawake na watoto ya kuishi salama.

Aliendelea kusema kwamba, kwa mujibu wa ripoti ya “Ukatili dhidi ya Watoto iliyotayarishwa na UNICEF, 2011”,ilibainisha kuenea kwa aina za ukatili wa kijinsia, kimwili na kiakili nchini Tanzania dhidi ya watoto na kuonesha kuna tatizo kubwa.

Alisema takribani asilimia 28 ya wasichana na asilimia 13 ya wavulana wamefikiwa na ukatili wa kijinsia kabla ya kutimiza miaka 18, zaidi ya asilimia 70 ya wasichana na wavulana wametendewa ukatili wa kimwili na zaidi ya robo wametendewa ukatili wa kiakili.

Adha alisema ripoti mbalimbali za haki za binadamu nchini zemebainisha kuna ongezeko kubwa la ukatili dhidi ya watoto kwa kipindi cha mwaka 2018 huku ongezeko kubwa la matukio ya ubakaji kwa waoto na wanawake yameripotiwa zaidi 2018 ukilinganisha na mwaka 2017.

Akizungumzia juu ya Kongamano hilo la kitaifa, alisema litafanyika Machi 21 na 22 katika ukumbi wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Dar es Salaam (DUCE) na linatarajiwa kuzinduliwa na Waziri Mkuu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa.

Alisema lengo kuu la kongamano hilo ni kuwapatia fursa viongozi wakitaifa, watafiti, asasi za kiraia, wataaluma na viongozi wa dini, wanaharakati wa haki za binadamu, vyombo vya habari, wanaume na wavulana, wanawake na watoto pamoja na wadau wa maendeleo kutoka ndani na nje ya nchi kujadili hali halisi ya ukatili pamoja na namna ya kuimarisha mikakati yakutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto.

Alisema kongamano hilo litaangazia pia mada kuu sita ambazo ni pamoja na hali ya ukatili kwa watoto katika familia na shuleni, ukatili wa kijinsia na unyanyasaji, mimba za utotoni, ndoa za utotoni, ukeketaji, malezi katika ulimwengu wa kisasa, ukatili wa kingono katika taasisi za elimu ya juu, ukatili dhidi ya watoto kwenye mitandao na namna yakuwapatia msaada wahanga wa vitendo vya ukatili.

Aidha alibainisha kwamba kongamano hilo limeandaliwa na CDF, chini ya udhamini wa Ubalozi wa Uswidi kwa kushirikiana na Shirika la C-Sema pamoja na Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Dar es Salaam (DUCE).