Mchezaji Wa Simba Jonas Mkude Akumbana Na Tatizo Zitto - The Choice

Mchezaji Wa Simba Jonas Mkude Akumbana Na Tatizo Zitto

0


HIVI karibuni, Jonas Mkude ameendelea kuthibitisha kwamba anastahili kuitumikia namba sita katika kikosi cha Simba.

Anaonyesha anastahili kwa kuwa amekuwa akiitendea haki namba hiyo kutokana na kuichezesha timu na pia kushiriki vema katika ukabaji.

Wakati fulani, baadhi ya makocha wa Simba hawakumkubali Mkude kutokana na upungufu kadhaa na huenda waliona kama vile haukuwa ukirekebishika na mwisho wakachukua uamuzi wa kumuweka nje.

Baadaye, presha ilikuwa kubwa kwa pande zote mbili, kuwa makocha wamchezeshe Mkude na baadaye kwamba Mkude akipewa nafasi aitendee haki.

Hakika Mkude anastahili pongezi angalau za awali kwa kuwa tangu amepewa nafasi amekuwa akifanya vizuri uwanjani na kuwa msaada kwa Simba na sisi tumeliona hilo namna ambavyo amekuwa akifanya.

Kawaida, rekodi zinaonyesha kwa asilimia 95, kila timu iliyochukua ubingwa katika Ligi Kuu England, maarufu kama EPL, ilikuwa na kiungo mkabaji bora aliyeweza kukaba na kuichezesha timu kwa pasi ndefu na fupi.

Kwa mfumo wa Kingereza, namba sita anakuwa na nafasi kubwa ya kuichezesha timu na kuanza kupanga mashambulizi kwa kuwa yeye anakuwa nyuma ya wengine isipokuwa kipa na walinzi wawili wa kati.

Utaona Roy Keane na Manchester United, Arsenal na Patrick Vieira, kwa siku za hivi karibuni angalia N’golo Kante na Leicester City na baadaye Chelsea.

Moja ya tatizo la kwanza la Mkude ambalo asingeweza kupata sifa ya kuwa msaada wa kuipandisha au kuisaidia timu kuanzisha mashambilizi ni pasi fupifupi za ‘shoo-shoo’. Lakini kwa sasa, mambo ni tofauti kwa kuwa amebadilika, sasa ni kati ya wachezaji wenye uwezo mkubwa wa kupiga pasi fupifupi zenye kutoa msaada kwenye kikosi hasa kinaposhambulia na amekuwa akipiga pasi ndefu pia ambazo awali zilikuwa zikimsumbua.

Kama lilikuwa ni tatizo la kiufundi, Mkude amemaliza. Lakini hili la nidhamu linaonekana kumshinda na ikiwezekana litamuangusha.

Hakuna mchezaji dunia hii amefanikiwa kwa kuwa na kipaji pekee. Hata uwe na kipaji bora kuliko wengine wote duniani, ukawa huna nidhamu basi ujue utafeli.

Waingereza wanasema ‘Character’, yaani tabia, ndiyo sumu kali ya ‘Talent’, yaani kipaji. Wapo ambao huvimba kichwa baada ya mafanikio madogo na tabia ikawaondoa njiani au wale ambao hata kabla ya kufanikiwa na harufu tu, wanajisahau na tabia mbaya inawaangusha.

Mkude alikuwa na tabia kadhaa ambazo niliwahi kuzizungumzia kwa kuandika makala na hakika nilifurahishwa kuona anabadilika.

Mabadiliko ya Mkude uwanjani yanaruhusu kupewa sifa, kupewa moyo na kuambiwa ashikilie alipo na baada ya hapo aendelee kuongeza juhudi na maarifa ili apige hatua.

Lakini tabia ambazo amekuwa akifanya anatakiwa kukemewa na kuelezwa kwamba mafanikio madogo aliyopata hadi sasa yasimsahaulishe. Tena kwa mtu ambaye anaonekana anategemewa, anapokosea jambo lake huchukuliwa kwa uzito wa juu.

Mkude sasa ni kati ya wale wa kikosi cha kwanza Simba, tabia za kuchelewa mazoezini, au kuchelewa ndege wakati kikosi kinaondoka hapaswi kuzifanya kwa kuwa ili kuonyesha uko makini lazima matatizo madogo kama hayo uyaondoe.

Ubora wa Mkude hauwezi kuwa uwanjani pekee, tabia bora kwa mchezaji ni ndani na nje ya uwanja na kawaida unapopewa nafasi lazima uwe mfano kwa unaofanya nao kazi na wale wanaochipukia.

Kuonyesha nidhamu pia ni kuonyesha unawathamini unaofanya nao kazi pia wale wanaokuunga mkono. Na mwisho unakuwa unawarahisishia kazi wale wanaokuongoza.

Mwalimu anaweza kuwa anatamani kukupanga kutokana na uwezo na msaada wako uwanjani. Lakini anashindwa kwa kuwa ni mtovu wa nidhamu na yeye amekuwa akisisitiza suala la nidhamu.

Hii inakuwa inampa wakati mgumu yeye kama kiongozi. Kumbuka kufanya mambo yaende vizuri inakuwa bora kufanya mambo sahihi kwa kuwa utawasaidia viongozi wako kuongoza kwa ulaini na sahihi.

Hakuna mjadala, Mkude hapaswi kuchelewa ndege au mazoezini. Mchezaji anayejitambua anajua namna ya kujipanga na muda wake ikiwemo kujipa nafasi ya muda wa kutosha kupumzika badala ya kutembea hovyo mitaani. Hii ni mara ya tatu namuandikia Mkude na msisitizo unakuwa ni palepale, akitaka kuwa bora zaidi lazima ayafukie mambo kadhaa hasa yale yanayohusiana na nidhamu.

Bado hajamaliza, yeye ni chipukizi na Simba si mwisho wa safari. Vema siku moja akipata nafasi akaenda nje ya Tanzania ambako nidhamu ni suala muhimu sana na linatazamwa kwa jicho la tatu.

Mkude aliwahi kuwa nahodha wa Simba na ana nafasi ya kuwa nahodha tena hapo baadaye. Hivyo nidhamu iwe nguzo hasa katika msingi badala kwenda ili mradi tu.

Share.

About Author