Mkwanja wa PSG wamng’oa Neymar Barca - The Choice

Mkwanja wa PSG wamng’oa Neymar Barca

0

PESA inaongea bwana, asikwambia tu. Barcelona inatikiswa kuhusu Mbrazili wake, Neymar na safari hii ngoma imekuwa nzito. Mbrazili huyo anachapa lapa.

Manchester United, Manchester City zimekuwa na uchokozi wa kumtaka fowadi huyo, lakini Paris Saint-Germain (PSG) ndiyo iliyovumisha upepo mbaya Nou Camp baada ya kuweka ofa ya maana mezani ambayo, Barca haiwezi kuchomoka.

Matajiri hao wa Ufaransa wameweka mezani dau nono la usajili pamoja na mshahara kwa ajili ya staa huyo, ambaye amevutika na ameweka bayana kuwa yuko tayari kutua PSG.

Ripoti zinabainisha kwamba Neymar, ambaye kwa sasa yupo mapumzikoni Marekani akila bata na mastaa wengine wa dunia akiwemo mcheza tenisi maarufu Seeena Williams, amedai kuwa klabu yake baada ya Barcelona itakuwa PSG.

UOL Esporte imefichua kwamba Neymar amekubali ofa ya mshahara mnono kutoka PSG na kwamba, atajiunga na matajiri hao kwenye msimu wa 2017-18.

Taarifa kutoka kwa mtu wa karibu wa mchezaji huyo imedai Neymar atakatisha mazungumzo yake na Barcelona na kuwaambia kwamba, atabaki hapo kwa msimu mmoja tu na kisha atakwenda Ufaransa.

Neymar na baba yake wanaamini uhamisho wa kwenda PSG utamfanya kwa haraka sana aweze kutambulika na kupewa thamani kwamba ni mchezaji mkubwa kabisa duniani.

Kutokana na hilo, msimu ujao Neymar ataendelea kuvaa jezi za Barcelona, lakini itakuwa kipindi chake cha mwisho klabuni hapo kutokana na kujiona kwamba, mahali hapo anafunikwa na wakali wengine, Lionel Messi na Luis Suarez.

PSG imeripotiwa kuwa itampa Neymar ofa ya kumlipa karibu Euro 50 milioni kwa mwaka ikiwemo mshahara na bonasi mbalimbali, kiasi ambacho ni zaidi ya nusu anachopata sasa kwenye mkataba mpya atakaopewa na Barcelona.

Mwaka jana Man United ilimweleza Neymar kwamba akijiunga na timu yao itamfanya kuwa staa mkubwa kwenye kikosi tofauti na Barcelona ambako itakuwa vigumu kwa upande wake kutokana na uwepo wa Messi.

Messi, Neymar na Suarez kwa msimu miwili sasa wameunda kombinesheni bora kabisa ya ushambuliaji katika kikosi cha Barcelona na kuwatesa wapinzani wao kwa kufunga mabao kwa kadiri walivyotaka.

Man United ikiwa chini ya Jose Mourinho kwa sasa na Manchester City chini ya Pep Guardiola zinaweza kurudi kwa kasi mpya kwenye usajili wa Neymar na kuipiku PSG, ambayo hadi sasa ndiyo inayoonekana kuwa mstari wa mbele kushinda vita ya kumnasa supastaa huyo wa Amerika Kusini.

Facebook Comments
Share.

About Author