Rasmi Okwi Afunguka Kuhusu Kujiunga Yanga ,Atoa Msimamo Juu ya Simba..!!! - The Choice

Rasmi Okwi Afunguka Kuhusu Kujiunga Yanga ,Atoa Msimamo Juu ya Simba..!!!

0
HATIMAYE kwa mara ya kwanza straika anayesubiriwa kwa hamu na Wanasimba, Emmanuel Okwi, amefunguka kuhusu uwezekano wa yeye kutua Msimbazi.
Okwi hivi karibuni amevunja mkataba wake katika kikosi cha Sonderjyske ya nchini Sweden aliyokuwa akiitumikia baada ya kujiunga nayo mwaka 2015.
Tangu avunje mkataba huo, gumzo kubwa limekuwa ni kuhusu kurejea kwake Simba huku Wanasimba wakimsubiri kwa shauku kubwa.
Wiki iliyopita, Klabu ya Sonderjyske ilitoa taarifa kuwa imeachana na Okwi ambaye tangu ajiunge na klabu hiyo hakuwa na nafasi ya kucheza katika kikosi chake cha kwanza, hivyo kuanzia sasa ni mchezaji huru na anaruhusiwa kujiunga na klabu yoyote itakayomhitaji.
Okwi, jana mchana akiwa nyumbani kwao Kampala, Uganda na ametamka kuwa hajafanya mazungumzo yoyote na Simba kama ilivyokuwa ikisemwa awali.
Ameeleza kuwa yupo nyumbani kwao ametulia na hakuna kiongozi yeyote aliyemfuata kuzungumza naye kuhusu mambo ya kimkataba.
Okwi ameenda mbali zaidi kwa kutamka kuwa hana mpango wowote wa kujiunga na Simba hivi sasa.
“Kwa sasa huo mpango sina na wala hamna makubaliano yoyote, mimi nilikuambiaga kama kuna lolote nitakuambia, lakini kwa sasa hakuna lolote na wala sina mpango huo,” alisema Okwi.
Okwi ambaye msimu wake wa mwisho Msimbazi (2014/15) alifunga mabao 10 na ambaye amekuwa akisifika kwa kuifunga Yanga, ameongeza: “Mimi nipo nimetulia zangu nyumbani, sitaki kuzungumza chochote hivi sasa kuhusu wapi nitakwenda. Kama tulivyozungumza wakati ule, mimi bado sijafanya mawasiliano yoyote na Simba,” alisema Mganda huyo.
Alipotafutwa Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia Hans Poppe, ili aweze kulitolea ufafanuzi suala hilo hakupatikana kutokana na simu yake ya mkononi kuita tu bila ya kupokelewa kama ilivyokuwa kwa katibu mkuu wa timu hiyo, Patrick Kahemele pamoja na mkuu wa kitengo cha habari na mawasiliano wa timu hiyo, Haji Manara.
Simba walikuwa na matumaini ya kumtumia Okwi katika mchezo dhidi ya Yanga, Februari 18, mwaka huu, ingawa baadaye ilikuja kubainika kuwa kanuni za TFF haziruhusu ingizo lolote wakati dirisha likiwa limefungwa, hata kama mchezaji ni huru, tofauti kabisa na kanuni za Fifa.
Simba inapambana kusaka ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu huu. Inaongoza ligi kwa tofauti ya pointi mbili tu dhidi ya wapinzani wao Yanga, hasa baada ya Simba kubanwa mbavu kwa sare ya 0-0 na Mtibwa Sugar katika mechi yake iliyopita.
Aidha, katika mchezo wa jana wakati wa Simba na Polisi Dar, mashabiki wa Yanga walimshangilia Mwenyekiti wa Usajili wa Simba, Zacharia Hans Poppe kwa kuimba: Okwi, Okwi, Okwi… alipokuwa akipita mbele yao wakati akielekea msalani kutoka jukwaa kuu alipokuwa amekaa kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar.
Facebook Comments
Share.

About Author