YANGA WAPO MBIONI KUWASAJILI WAWILI KUTOKA GHANA - The Choice

YANGA WAPO MBIONI KUWASAJILI WAWILI KUTOKA GHANA

0
KUFUATIA kuondoka kwa kiungo wao, Haruna Niyonzima, klabu ya Yanga imeamua kupotezea na sasa kuelekeza nguvu zao kwa wachezaji wengine wa kimataifa, ambapo wana mpango wa kusajili mastaa wawili wa Ghana.
Pamoja na Niyonzima, mchezaji mwingine wa Yanga ambaye anadaiwa kuwa njiani kuelekea kwa mahasimu wao, Simba ni mshambuliaji wao, Donald Ngoma, huku Obrey Chirwa akidaiwa kuomba kuvunja mkataba na klabu hiyo.
Wakati mpachika mabao wao, Amis Tambwe akitaka dau kubwa ili aongeze mkataba mpya, Justine Zulu ametemwa na Wanajangwani hao kutokana na kushindwa kuonyesha uwezo uliotarajiwa.
Kufuatia kung’atuka kwa wachezaji hao, Yanga imeamua kusaka mbadala wa wachezaji hao wanaoondoka, huku BINGWA likijulishwa kwamba tayari Yanga imefanya mazungumzo na mshambuliaji wa Inter Allies FC, Martin Antwi pamoja na beki wa Asante Kotoko, Amos Frimpong.
Frimpong, ambaye pamoja na kucheza beki wa kulia lakini pia ana uwezo wa kukipiga beki wa kati, anaweza kuja kuwa msaada mkubwa kwa timu hiyo kwa nafasi hiyo ya ulinzi, ambayo pia huenda ikaondokewa na beki wa Togo, Vicent Bossou.
Nahodha huyo wa Asante Kotoko mwenye uwezo mkubwa wa kukaba na kucheza kwa nguvu, huenda ikawa dawa tosha kwa washambuliaji wasumbufu kama Emanuel Okwi, ambaye anatarajiwa kutua Simba.
Antwi, mwenye umri wa miaka 23, ni mzuri sana kwenye kutingisha nyavu na ana uwezo wa kufungasha mabeki hata watatu, akitumia vizuri mguu wake wa kushoto.
“Uongozi upo kwenye mazungumzo na wachezaji hao na kama mambo yatakwenda vizuri, basi watamalizana nao na kuonekana msimu ujao wakiwa na uzi wa Yanga,” kilisema chanzo cha habari.
Wakati huo huo, kuna taarifa kwamba uongozi wa Yanga umemtaka kocha wa timu yao, George Lwandamina, kuja na wachezaji wawili wa kimataifa, ambao anaona wanaweza kufiti kwenye kikosi chake.
Share.

About Author